Kwa nini tiba mbadala ni tishio kwa wagonjwa wa saratani
Na MARY WANGARI
WAGONJWA wa saratani wametahadharishwa dhidi ya kukatiza matibabu wanayopatiwa na madaktari hospitalini na kuanza kutumia tiba mbadala wakionywa kufanya hivyo kunavuruga uwezekano wao wa kupona.
Akizungumza katika mkutano kimtandao ulioandaliwa Nairobi mnamo Jumatatu, Oktoba 5, Daktari Catherine Nyongesa ambaye ni mtaalam kuhusu maradhi ya saratani katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH), alisema haijathibitishwa kisayansi kuwa dawa mbadala kama vile mitishamba zinaweza kuponya saratani.
“Kwa sasa hakuna dawa za kiasili ambazo zimethibitishwa kuwa na uwezo wa kutibu saratani. Ni muhimu kufuata maagizo ya matibabu utakayopatiwa hospitalini ili kuhakikisha kwamba hautatizi mchakato wa tiba,” alisema Dkt Nyongesa.
Kulingana na mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Saratani Kenya (KENCO), Catherine Wachira, kumekuwa na visa kadhaa vya wagonjwa wanaokatiza matibabu wanayopatiwa hospitalini na kuanza kutumia dawa za kienyeji kwa dhana kuwa zinafaa zaidi.
“Tunawahimiza wagonjwa wa saratani wajiepushe na kukatiza matibabu wanayopatiwa na madaktari na kuanza kutumia tiba mbadala,”
“Hii ni kwa sababu kufanya hivyo kunavuruga mchakato wa matibabu na kufanya iwe vigumu kwa mgonjwa kupona,” alisema Bi Wachira.
Wakati huo huo, Dkt Nyongesa aliwahimiza wanawake pamoja na wanaume waliosonga kiumri kujitokeza na kwenda kupimwa saratani ya matiti akisema kuwa kugunduliwa mapema kwa ugonjwa huo humwezesha mgonjwa kuanza matibabu haraka hivyo kuwa nafasi bora zaidi ya kupona.
Aidha, aliwahimiza wanawake wasiogope kupimwa na wahudumu wa afya wa jinsia tofauti akisisitiza kwamba wauguzi wa kiume ni wataalam wanaofahamu kazi yao na wanaongozwa na kanuni za kitaaluma.
“Wanawake hawafai kuogopa kupimwa saratani ya matiti. Ukiwa na umri wa zaidi ya miaka 35 unaweza kufanyiwa mamogramu. Ni asilimia chache tu ya vipimo vinavyotokea kuwa na saratani hivyo hakuna haja ya kuogopa,”
“Wanaume waliosonga kiumri pia ni muhimu waende kufanyiwa vipimo kwa sababu wao pia wamo katika hatari ya kupata gonjwa hilo,” alisema.
Alifafanua kuwa saratani ya matiti inaweza kuathiri wanawake na hata wasichana wenye umri mchanga ikizingatiwa kuwa mambo kadhaa yanachangia ikiwemo unywaji pombe, uvutaji sigara, masuala ya jeni, uharibifu wa mazingira, kemikali miongoni mwa mambo mengine.