Habari Mseto

LAMU: Ziwa Kenyatta lililokauka sasa lajaa maji

December 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

MIAKA miwili baada ya Ziwa Kenyatta linalopatikana kwenye tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu kugonga vichwa vya habari kufuatia kukauka kwake ghafla, hatimaye ziwa hilo limepata uhai tena baada ya kujaa maji.

Ziwa hilo ambalo ni la kipekee kwa kuhifadhi maji safi ambayo si ya chumvi lilipewa jina la mwanzilishi wa taifa hili, Mzee Jomo Kenyatta.

Ziwa hilo linategemewa na watu zaidi ya 60,000 na mifugo zaidi ya 200,000 inayoishi eneo hilo.

Kati ya mwaka 2016 na 2017, Ziwa Kenyatta lilikauka kufuatia ukame wa muda mrefu, hivyo kupelekea makumi ya viboko waliokuwa wakiishi ndani ya ziwa hilo kufariki.

Mamia ya ndege, konokono wa majini na samaki pia walifariki punde ziwa hilo lilipokauka, hatua ambayo ilichafua kabisa mazingira ya ziwa hilo, hivyo kufanya hewa kunuka shombo.

Taifa Leo ilipozuru kwenye ziwa hilo Jumatatu, hali ilikuwa tofauti ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita kwani harufu mbaya haipo tena.

Maandhari ya Ziwa Kenyatta sasa ni ya kupendeza kwani vipepeo walionekana wakirukaruka angani, ndege wakiimba nyimbo za furaha na kijani kibichi kikitanda kote.

Ama kweli, uhai umerejea Ziwa Kenyatta. Picha/ Kalume Kazungu

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Mwenyekiti wa Shirika la Kudhibiti Hadhi ya Ziwa Kenyatta, Bw Kamau Githu alishukuru mvua kubwa iliyoshuhudiwa kote nchini na hata kusababisha mafuriko kwenye baadhi ya maeneo ya kaunti na nchi kati ya Aprili na Agosti mwaka huu.

Bw Githu anasema mvua hiyo ndiyo iliyochangia kuleta uhai tena kwenye Ziwa Kenyata.

“Matumaini ya ziwa letu kwamba lingerejelea hali yake ya kawaida yalikuwa yamefifia kabisa. Mvua kubwa iliyonyesha nchini kati ya Aprili na Agosti mwaka huu ndiyo iliyosaidia kujaza maji upya kwenye ziwa hilo. Kwa sasa mazingira yanavutia ziwani kwani wanyama na ndege wa kila aina wamerejea tena Ziwani Kenyatta,” akasema Bw Githu.

Afisa huyo aidha alieleza kuwa hali bado ni ya kutiliwa shaka ziwani kwani baadhi ya wanyama wakubwa, ikiwemo viboko na nyati na hata aina nyingine ya samaki walipotea kabisa tangu ziwa hilo lilipokauka.

“Maji yapo lakini kina chake ni kidogo ikilinganishwa na awali. Maji ya Ziwa Kenyatta yalikuwa na kina cha mita 12 wakati ziwa likiwa limejaa pomoni. Leo hii maji yako na urefu wa kina cha mita 6 pekee. Hii ni kwa sababu kuna mchanga mwingi chini ya ziwa na hili limesababisha wanyama wakubwa kama viboko na hata aina fulani ya samaki waliokuwepo ziwani kutoroka,” akasema Bw Githu.

Naye Mwenyekiti wa Muungano wa Watumiaji Maji na Rasilimali zipatikanazo Ziwa Kenyatta, Bi Susan Gaitho, alitaja shughuli mbalimbali zinazoendelezwa na wakazi kando ya Ziwa Kenyatta, ikiwemo ukulima na ufugaji kuwa kero kwa uhifadhi wa ziwa hilo.

Bi Gaitho alisema shirika lake tayari limeanzisha hamasa kwa wakazi kuepuka kuendeleza kilimo kando ya ziwa hilo na pia kukomesha wafugaji wanaopeleka mifugo wao kunywa maji moja kwa moja kwenye ziwa hilo.

Aliwataka wadau mbalimbali na mashirika ya mazingira kujitokeza ili kusaidia kudhibiti hadhi ya Ziwa Kenyatta.

“Ukulima umechangia mmomonyoko wa udongo ambao huteremka chini na kulijaza tako la ziwa. Licha ya kwamba ziwa linaonekana kujaa pomoni, maji bado ni kidogo kwani kina chake ni kifupi mno. Hii imepelekea maji kuyeyuka kwa urahisi kutoka ziwani hasa msimu huu wa kiangazi. Kuna haja ya wadau kushikana na kulichimba ziwa zaidi ili mvua ikinyesha maji yawe na mahali pakubwa pa kuingia,” akasema Bi Gaitho.

Mwanaharakati wa Mazingira eneo la Mpeketoni, Samuel Muchiri, aliiomba kaunti na serikali ya kitaifa kuleta wataalamu watakaokagua na kutathmini hali ya Ziwa Kenyatta na kutafuta mbinu zitakazohakikisha hadhi ya ziwa hilo inadhibitiwa kikamilifu siku za usoni.