Lango la JKIA kufungwa Melania Trump akitarajiwa kutua nchini
Na BERNARDINE MUTANU
Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege nchini (KAA) Alhamisi imetangaza kuwa Ijumaa itafunga lango la pili la uwanja wa ndege wa JKIA, (Terminal 2) kati ya saa kumi na moja na nusu jioni hadi saa tatu usiku.
Hii ni kutokana na ziara yake mkewe Donald Trump, Melania, anayetarajiwa kuzuru humu nchini. Pia, lango hilo litafungwa tena Oktoba 6 kutoka saa sita za usiku hadi saa tatu za asubuhi kulingana na tangazo lililochapishwa Jumatano.
“Wakati huo, operesheni zote za ndege za humu nchini zinazoendeshwa T2 zitaendeshwa katika T1D. Terminal 1E itatumika kwa wote wanaofika nchini kutoka mataifa mengine na terminal 1B itatumika na wote wanaoondoka nchini,” ilisema KAA katika tangazo hilo.
“Abiria wanashauriwa kufika JKIA takriban saa tatu kabla ya muda wa kuondoka nchini ili kutoa muda unaotosha kwa ukaguzi wa usalama,” ilisema notisi hiyo.
Bi Trump atatembea katika Ukumbi wa Kitaifa wa Maonyesho na kutembelea nyumba kadhaa za watoto Jijini Nairobi.
Alikuwa Ghana kabla ya kufika Kenya na anatarajiwa kusafiri hadi Malawi na Misri katika ziara yake ya mwanzo akiwa peke yake nje ya Marekeni.