Habari Mseto

Lawama tele makamishna wa NLC wakiondoka afisini

February 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

TUME ya Ardhi Nchini (NLC) iliondoka afisini Jumanne, japo ikiandamwa na lawama nyingi kutoka kila upande za kukosa kutekeleza wajibu wake jinsi ilivyotarajiwa.

Makamishna wa tume hiyo walikuwa na kibarua kigumu kujitetea mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Ardhi, wakati wabunge waliilaumu vikali kuhusu mizozo mingi ya ardhi ambayo ilishindwa kutatua.

Wabunge vilevile walieleza kughadhabishwa kwao na mwenyekiti wa tume hiyo Muhammad Swazuri, ambaye walisema amekuwa akikwepa kufika mbele ya kamati hiyo kueleza kuhusu masuala mengi ya utendakazi wa tume na kufanya kazi kwa njia zisizopendeza.

Wabunge wengi walidai kuwa kamati hiyo badala ya kushughulikia kesi nyingi kuhusu mizozo ya mashamba miongoni mwa maelfu ya Wakenya imekuwa ikijishughulisha na mizozo inayohusisha mabwanyenye ambapo maafisa wake wanajinufaisha kwa namna fulani, huku Wakenya maskini wakiachwa kwenye matatizo.

“Tume hii imekuwa tu ikikimbizana na mizozo ya ardhi ambapo kuna ‘dili’ na kuwaacha Wakenya maskini ambao wana matatizo ya ardhi bila suluhisho. Vilevile, mwenyekiti wa tume amekuwa akikwepa kufika mbele ya kamati za bunge,” akasema mwakilishi mwanamke wa kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru.

Hata jana, Bw Swazuri hakufika mbele ya kamati hiyo ya bunge, ila ni makamishna wengine waliofika, wakiongozwa na naibu mwenyekiti, Bi Abigael Mbagaya.

Kutoka kulia: Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NLC Bi Kabale Tacha, aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa NLC Abigael Mbagaya mbele ya Kmati ya Bunge kuhusu Ardhi Februari 19, 2019. Picha/ Peter Mburu

Bi Mbagaya, hata hivyo, alitetea tume hiyo kuwa ilijikaza kutekeleza majukumu yake kadri ilivyoweza, japo akisema mazingira yalikuwa magumu na ufadhili usiotosheleza kutoka kwa serikali.

“Kama tume, tumetimiza wajibu wetu na kutekeleza kazi kama Wakenya walivyotaka. Tumefanya vyema tuwezavyo kulingana na hali ngumu tuliyokuwa tukifanyia kazi,” akasema afisa huyo. Jana ilikuwa siku ya mwisho kwa tume hiyo kuwa afisini.

Bi Mbagaya alisema japo NLC inahitaji wafanyakazi 1100 ili kutekeleza majukumu iliyopewa kikatiba iwezekanavyo, imekuwa na wafanyakazi 450 pekee.

Alikiri kuwa bado kuna maelfu ya hati za umiliki wa ardhi za umma ambazo bado ziko katika mikono ya watu binafsi wasiofaa na ambazo zinafaa kuharamishwa.

Lakini kila takriban kila mbunge aliyezungumza aliilaumu tume hiyo, haswa mwenyekiti wake kuwa walifeli kutekeleza majukumu yao.

“Kwanza kama Bw Swazuri hapatikani kabisa hata ukienda katika afisi yake, anajua kukwepa sana. Ikiwa tume hii itaendelea kufanya kazi jinsi inavyofanya sasa, huenda tukachukua miaka 150 kusuluhisha mizozo ya ardhi ya tangu jadi,” mbunge wa Kajiado Magharibi George Sunkuyia akasema.

Aliungwa mkono na mbunge wa Soy Caleb Kositany ambaye alisema tume hiyo imekuwa ikifanya kazi kuwaridhisha matajiri tu, ilhali masikini wanalia.

Jana ilikuwa siku ya mwisho kwa tume hiyo kuwa afisini japo mwenyekiti wake Bw Swazuri hakuwepo, kwani amekuwa akikumbwa na kesi kortini.

Bi Mbagaya alisema kuna amri ya korti ya kumzuia Bw Swazuri kutangamana na mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo na akaongeza kuwa makamishna ni mashahidi.

Aidha, Bi Kabale Tacha sasa ndiye atakuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa NLC kufuatia muhula wa tume ya sasa kukamilika.