LSK yaonya kuhusu hatari ya kusafiria gari lisilo na bima
NA MWANGI MUIRURI
RAIS wa Muungano wa Wanasheria katika Kaunti ya Murang’a Bw Alex Ndegwa ameonya wenyeji dhidi ya kukodisha magari yasiyo na bima halali kufika kwa sherehe zao.
Alisema kwamba kaunti hiyo imejaa visa ambapo wananchi wamehusika kwenye ajali wakitumia magari ya kukodisha yasiyo na bima halali, na kuishia kukosa kufidiwa.
“Watu waache kucheza kamari na maisha yao. Tukome huu mtindo wa kupewa lifti au kukodisha magari yasiyo na bima,” akasema.
Bw Ndegwa akiongea katika kongamano la uhamasishaji katika Mkahawa mmoja Murang’a mnamo Machi 16, 2024 alisema kwamba “abiria akipata ajali katika gari lisilo na bima ni sawa tu na kujiua ambapo hutapata fidia”.
Alisema wanachofanya maafisa wa usalama, ni kumkamata dereva au mmiliki wa gari, hilo ikiwa hakuaga dunia na wamshtaki kwa makosa ya kuendesha gari bila bima au leseni.
“Wakati kuna mauti ndani ya ajali hiyo, dereva huyo atashtakiwa kwa makosa ya kuuza na kusababisha majeruhi lakini fidia kwa waathiriwa itakosa,” akasema Bw Ndegwa.
Alisema njia nyingine ya kutafuta fidia ni kupitia kumshtaki mwenye gari hilo katika mahakama ya kutatua migogoro ya kibiashara ili mmiliki au dereva alipe fidia kama mtu binafsi, njia ambayo alisema ni ndefu na tata.
Kukwepa utata huo, Bw Ndegwa alisema kwamba “Ni jukumu la abiria wajifahamishe na masuala ya bima na wawe wakihakikisha kwamba wanaabiri tu yale yaliyojisajili kihalali”.
Aliwataka raia wawe wakikataa kutumia njia za mkato kufika waendapo.