LSK yashtaki utekelezaji wa agizo la magari jijini
NA MAUREEN KAKAH
MAWAKILI wanataka amri ya kuzuia magari kuingia katikati mwa jiji la Nairobi kwa siku mbili kila wiki, maarufu kama “Car Free Days” isitekelezwe hata baada ya kukamilishwa kwa usajili wa kielektroniki wa wachuuzi wanaotarajiwa kutumia siku hizo kuuza bidhaa zao.
Chama cha mawakili (LSK) mnamo Ijumaa kiliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu kikishtaki Wizara ya Uchukuzi, serikali ya Kaunti ya Nairobi na Mwanasheria Mkuu, kikisema amri hiyo ilitolewa bila mashauriano na hata kabla ya mabasi makubwa ya uchukuzi kuletwa nchini.
Kwenye stakabadhi zao za kesi, mawakili hao wanafafanua kwamba kuna ofisi za watu binafsi na wakuu wa serikali, hospitali na taasisi za kielimu ambazo lazima zifikiwe na wahusika wakitumia magari yao, na hivyo kuwazuia kufanya hivyo ni kuwanyima uhuru wao.
LSK pia inadai kwamba wenye biashara ambao wamelipia leseni za kuhudumu jijini watapata hasara kubwa.
Chama hicho kinadai kwamba walemavu wataathirika zaidi kwa sababu hakuna maelezo hadi sasa kuhusu namna watakavyoshughulikiwa kufikia maeneo yao ya kazi. Masaibu hayo pia yatawapata watoto wadogo ambao hupelekwa shuleni kwa magari ya kibinafsi na kuchukuliwa na wazazi wao kila siku.
“Wanaposisitiza nia yao ya kutekelezwa amri hiyo, washtakiwa wamekosa kutoa njia mbadala ya uchukuzi ambazo zitahakikisha haki na maisha ya watu watakaoathirika moja kwa moja zinalindwa,” akasema wakili Eddie Omondi anayewakilisha LSK.
Wakili huyo alifichua kwamba mara tu amri hiyo ilipotolewa mwezi jana, LSK iliandikia washtakiwa baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa umma, lakini wakakosa kujibiwa ndiyo sababu hawakuwa na lingine ila kuwashtaki mahakamani.
Amri iliyoyazuia magari ya umma na kibinafsi kuingia jijini siku za Jumamosi na Jumatano, ambayo ilifaa kutekelezwa kuanzia Februari 1, ilisitishwa kwa muda mnamo Januari 30 ili kuruhusu shughuli za usajili wa wafanyabiashara kielektroniki kukamilika.