Lumumba asema alihudumiwa kwa heshima aliponyimwa kuingia nchini Zambia
Na WALTER MENYA
MSOMI maarufu wa sheria nchini Prof PLO Lumumba amekanusha kuwa tisho kwa yeyote baada ya kunyimwa kibali cha kuingia nchini Zambia mnamo Jumamosi.
Prof Lumumba alizuiwa kuingia nchini humo na maafisa wa uhamiaji kwa kile walichosema kuwa sababu za kiusalama.
Ujumbe uliotolewa na Waziri wa Habari za Zambia, Dora Siliya ulisema kuwa hatua hiyo ilitokana na haja ya kuhakikisha usalama wa Zambia haivurugwi.
“Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imemyima Prof Lumumba kibali cha kuingia kutokana na sababu za kiusalama. Idara hiyo yetu ya usalama inashirikiana na zingine ndani na nje ya Zambia kuhakikisha kuwa hali ya usalama imedumishwa,” akasema waziri, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali.
Hata hivyo, msomi huyo alijitetea akisema kuwa huwa anasafiri kote barani Afrika bila vikwazo vyoyote.
“Mimi si tisho kwa yeyote. Huwa nasafiri kote barani Afrika,” akasema.
Vile vile, alisema kuwa licha ya masaibu hayo, idara hizo zilimshughulikia kwa heshima.
Vyombo vya habari nchini humo vilisema kuwa msomi huyo aliambiwa aondoke mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kenneth Kaunda.
Kulingana na gazeti la Lusaka Times, Prof Lumumba alipangiwa kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Eden kuhusu mkondo wa uhusiano wa kisiasa kati ya Uchina na Afrika.
Uchina ndiyo mwekezaji mkubwa zaidi nchini humo, huku kandarasi nyingi zikitolewa kwa kampuni zake.
Miongoni mwa miundomsingi inayojengwa na China nchini Zambia ni barabara, reli, viwanja vya ndege, viwanda kati ya mingine.
Zambia imekumbwa na msukosuko wa madeni inayodaiwa na China, na katika siku za majuzi kumekuwa na mijadala ya uwezekano wa China kuchukua usukani wa baadhi ya miundomsingi ya Zambia ili kujilipa madeni yake.
Hali kama hiyo ilifanyika kwa nchi ya Sri Lanka baada ya China kutwaa bandari yake.