Lusaka aonya MCAs dhidi ya kupapia kurekebisha Katiba
Na DENNIS LUBANGA
SPIKA wa Seneti, Bw Ken Lusaka ameonya madiwani dhidi ya kupapia kujihusisha na masuala ya kurekebisha Katiba akisema watakuwa hatarini kuathiriwa zaidi na marekebisho yanayopendekezwa.
Akizungumza katika duka la jumla la Rupa mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, aliomba madiwani watafute ushauri kwa mapana na marefu kabla ya kufanya maamuzi kuhusu marekebisho hayo.
“Kuna mijadala inayoendelea kuhusu marekebisho ya Katiba. Ombi langu kwa madiwani ni kwamba, msiharakishe kujihusisha kwa michakato hiyo. Badala yake, tuchukue muda, tusome na tuelewe manufaa ya marekebisho yanayopendekezwa kwa raia wa kawaida,” akasema.
Alikuwa amehudhuria hafla ya kufunga mashindano ya michezo ya Muungano wa Spoti wa Mabunge ya Kaunti (CASA).
Pendekezo la kurekebisha Katiba kutoka kwa Chama cha Thirdway Alliance kinachoongozwa na Dkt Ekuru Aukot, limekataliwa katika kaunti nyingi ambako aliwasilisha kwa madiwani bungeni.
Ijapokuwa Kiongozi wa ODM Raila Odinga pia hutaka kuwe na marekebisho ya Katiba, ingali inasubiriwa kuonekana iwapo jopokazi la maridhiano (BBI) alilounda na Rais Uhuru Kenyatta litapendekeza kura ya maamuzi.
Kwa upande mwingine, Baraza la Magavana pia lilianzisha mchakato wa Ugatuzi Initiative ambapo hitaji lao kuu ni kwamba kaunti iongezewe rasilimali kutoka kwa Serikali Kuu.
Kuangamiza ugatuzi
Bw Lusaka ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa Bungoma, alisema madiwani wakiendelea kujihusisha katika mijadala ya kurekebisha Katiba kiholela, kutakuwa na hatari ya kuangamiza ugatuzi sawa na jinsi ilivyofanyika enzi za Majimbo.
“Mfumo wa uongozi wa Majimbo ulisambaratika miaka ya sitini kwa sababu haukueleweka vyema. Kama hatutajihadhari, ugatuzi pia utaangamia vivyo hivyo,” akasema.
Aliahidi kwamba seneti itajitolea kusaidia mabunge ya kaunti na akataka madiwani watekeleze jukumu lao la kuhakikisha magavana wanatumia vyema rasilimali za kaunti.
Vile vile, aliomba kamati za mabunge ya kaunti kushirikiana na seneti ili kuimarisha ugatuzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bw Wycliffe Oparanya alisema kaunti zimeonyesha uwezo wa kuleta umoja kitaifa kupitia kwa maandalizi ya michezo inayoleta pamoja kaunti mbalimbali.