Maafikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Nakuru na wahudumu wa matatu bado ni ndoto
Na JOSEPH OPENDA
HAKUNA ishara zozote za mapatano wala maafikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Nakuru na wahudumu wa magari ya uchukuzi ya matatu baada ya serikali ya kaunti hiyo kufanya maamuzi ya kuhamisha wahudumu hao kutoka katikati mwa mji.
Huku Gavana Lee Kinyanjui akifutilia mbali uwezekano wowote wa kubatilisha maamuzi yake ya kupiga marufuku matatu kwenye eneo la CBD, wahudumu wa magari hayo ya uchukuzi wa umma wameapa kutotamauka katika jithada za kurejelea shughuli zao katikati mwa mji.
Mnamo Septemba 28, 2020, wahudumu wa matatu waliandamana katikati mwa mji na viungani mwake kwa zaidi ya saa tano huku wakimkashifu Gavana Kinyanjui kwa matamshi yake kwamba megenge ya wahalifu na magaidi yalikuwa yametwaa uendeshaji wa sekta ya matatu.
Kwa mujibu wa Gavana Kinyanjui, wengi wa waandamanaji waliishia kuzua vurugu, kusitisha shughuli za kibiashara mjini, Kuharibu mali na kufunga barabara – jambo lililokwaza shughuli za usafiri kwa kipindi kirefu.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Matatu kutoka Bonde la Ufa, Steve Muli, wahudumu wa matatu walimlaumu Gavana Kinyanjui kwa ubaguzi ikizingatiwa kwamba aliwakubalia wachuuzi kuuza bidhaa zao katikati mwa mji wa Nakuru huku wao wakipigwa marufuku.
Kwa mujibu wa Muli, eneo walikohamishiwa halina mazingira bora ya kufanyia biashara, linakosa huduma muhimu za usafi kama vile maji na vyoo na lina visa vingi vya utovu wa usalama.
“Baadhi ya wateja wetu ni walemavu, wagonjwa na wanawake wajawazito. Kufikia mahali pa kuabiri matatu au kufikia huduma muhimu baada ya kushuka garini ni vigumu sana,” akasema Muli.
Hata hivyo, Gavana Kinyanjui ameshikilia kwamba maamuzi hayo yalifanywa na serikali yake kwa minajili ya kuboresha utolewaji wa huduma muhimu katikati mwa mji, kuimarisha usalama na kudumisha usafi wa mji wa Nakuru.
Katika taarifa yake, Gavana Kinyanjui amewahimiza washikadau wa sekta ya uchukuzi mjini Nakuru kuunga mkono mipango yake ya maendeleo badala ya kutumiwa vibaya na wanasiasa wanaohujumu juhudi zake za maendeleo.
“Tulipoandaa mkutano na viongozi wa wahudumu wa matatu, wale walijotokeza mkutanoni ni wanasiasa na ‘wahudumu bandia’ waliotumiwa vibaya na wanasiasa waliokuwa na azma kutumia kikao hicho kama jukwaa la kujiendeleza kisiasa,” akasema Gavana Kinyanjui.
IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO