• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
‘Maafisa wa afya ya umma ni wachache nchini’

‘Maafisa wa afya ya umma ni wachache nchini’

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA upungufu wa maafisa wa afya ya umma nchini na wanastahili kuongezeka zaidi, amesema Mwenyekiti wa Idara ya Afya ya Umma na Kamati ya Kiufundi, Bw Simon Kimani.

Alisema uchunguzi uliofanywa hivi majuzi ulibainisha ya kwamba maafisi walioko ni wachache ambapo hawawezi kutosheleza mahitaji ya umma kote nchini.

“Tunastahili kuwapata maafisa wengi wa afya ya umma hapa nchini ili waweze kuhudumia wananchi kikamilifu katika maeneo ya mashinani. Nasema hayo kwa sababu kuna shida kubwa,” alisema Bw Kimani.

Aliyasema hayo Ijumaa katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya alipokutana na wahadhiri na wanafunzi.

Alifafanua ya kwamba kwa wakati huu kuna maafisa wa afya ya umma wapatao 4,000 kote nchini ambao wametwikwa jukumu la kuhudumia takribani idadi ya watu 45 milioni.

“Hilo ni jambo la kushangaza sana kwa sababu inamaanisha ya kwamba kila afisa atalazimika kuhudumia watu wapatao 11,250,” alisema Bw Kimani.

Alisema serikali ina kibarua kikubwa kuwapata maafisa wa kutosheleza mahitaji ya wananchi kote nchini.

Alizidi kueleza ya kwamba nchi hii inahitaji tena maafisa wengine kama hao 4,000 ili angalau kutumikia wananchi kwa njia bora zaidi.

“Kwa wakati huu tunapitia masaibu mengi kuhusiana na maswala ya mazingira. Tungetaka maafisa wa afya ya umma wawe wakizuru mashinani ili kutatua matatizo yanayoshuhudiwa nchini,” alisema Bw Kimani.

Matatizo

Allieleza kwamba maafisa hao wanastahili kusambazwa katika Serikali za Kaunti ambako kuna matatizo yanayoshuhudiwa kila mara na wananchi.

Alisema majukumu yao hasa ni kutazama maswala ya majitaka, afya ya umma katika mazingira, uzoaji wa taka katika makazi, uhifadhi wa chakula, na kuweka mazingira kuwa safi kila mara.

Alisema maafisa wanaostahili kupelekwa mashinani ni sharti wawe wenye ujuzi kamili wa kutenda kazi kwa ustadi ili kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Alizidi kufafanua kuwa watazidi kuboresha utendakazi wa maafisa hao ili wanapoendesha majukumu yao wawe watu waliobobea katika taaluma hiyo.

Naibu Chansela wa MKU Profesa Stanley Waudo alisema hivi karibuni watazindua masomo ya uzamili na uzamifu katika taaluma ya afya ya umma ili kuwapata maafisa wenye ujuzi kamili watakaoendesha majukumu yao kwa weledi wa hali ya juu.

“Tunataka kuona ya kwamba nchi yetu inapiga hatua katika uboreshaji wa maswala ya afya ya umma kwa kuwa na maafisa wenye ujuzi wa hali ya juu ambao wataweza kukubalika katika ulimwengu mzima,” alisema Prof Waudo.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Mara moja tu, naitupa’

UMBEA: Usikilize moyo wako ikiwa unapitia huzuni ya mahaba

adminleo