Habari Mseto

Maafisa wa utawala wawapeleka shule watoto 56

January 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SAMMY KIMATU

WANAFUNZI 56 kutoka familia za kipato cha chini ambao walibakia nyumbani baada ya kukosa karo ya kujiunga na Kidato cha Kwanza, wana kila sababu ya kutabasamu baada ya maafisa wa utawala kuwalipia karo na sare za shule.

Naibu kamishna wa Starehe John Kisang alithibitisha kwamba wasaidizi wa kamishna South B, Mabw Solomon Muranguri na Kimeu Ndambuki wameshirikisha chifu wa lokesheni ya Mukuru-Nyayo Paul Muoki Mulinge na Naibu Chifu Vincent Ambuga kupiga jeki watoto hao kielimu.

Bw Kisang aliongeza kwamba machifu hao walishirikiana na kamati za Nyumba Kumi, na viongozi wa mitaa kuwatambua watoto ambao hawakuweza kuendelea na masomo baada ya kufanya KCPE 2023 na kukosa karo.

“Ni kweli watoto hawa ni baadhi tu ya wengi wanaolemewa na umaskini katika mitaa ya mabanda ilio ndani ya tarafa ya South B. Machifu wangu na wasaidizi wangu wamefanya jambo nzuri zaidi kutafuta wasamaria wema kugharamia elimu ya watoto 56,” Bw Kisang asema.

Aliongeza kwamba wanafunzi hao walijiunga katika shule ya kutwa iliyo ya serikali ya Nairobi South Secondary.

Vilevile, Bw Kisang alisema maafisa hao wa utawala walipata ufadhili kutoka kwa wahisani wa kibinafsi na kutoka kwa shirika la Kijamii la Darul Kheir linaloongozwa na kinara Bi Aisha Mohammed almaarufu Soma Mama.

Wakati huo huo, Bw Kisang aliongeza kwamba wanafunzi hao hawatalipa ada ya dawati na kiti baada ya mbunge wa Starehe Amos Mwago kugharimia malipo hayo.

Isitoshe, wanafunzi hao walikuwa ni mseto wa waliozoa alama kuanzia 146 na 305 katika KCPE 2023.

Kwa mujibu wa meneja wa Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo bunge (NG-CDF), Daudi Obonyo Bw Mwago yuko tayari pia kuwapatia basari wanafunzi wote 56 mnamo Alhamisi.

Shule ya sekondari ya Nairobi South ndiyo ya kipekee ya serikali kupatikana katika tarafa ya South B.

“Kufikia Januari 20, 2024, katika Kidato cha Kwanza, idadi ya wanafunzi ilikuwa 152 lakini hadi Jumanne, tuna watoto 208. Kwa jumla ni shule iliyo na wanafunzi 554 kwa sasa,” Bw Muranguri akaambia Taifa Leo.

Alikumbusha wazazi kwamba serikali haijabatilisha sheria kwamba ni lazima kila mzazi apeleke mtoto shuleni na kuonya kwamba watakamatwa (wazazi) wakipatikana wamekaa nyumbani na watoto bila watoto kuwa darasani wakipata elimu.

“Serikali inatilia mkazo mpito wa asilimia moja wa elimu. Lazima kila mtoto awe shuleni akisoma. Mzazi ambaye atapatikana na mtoto nyumbani badala ya kumpeleka kusoma atakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria,” Bw Muranguri akaonya.

[email protected]