Maafisa waimarisha vita kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya Kwale
Na MISHI GONGO
KAMANDA wa polisi katika Kaunti ya Kwale Bw Joseph Nthenge amesema kuwa wamezindua upya vita dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya.
Alisema ulanguzi huo umekithiri katika Pwani ya Kenya lakini akaahidi kuwa watashirikiana na washikadau wengine kuhakikisha kuwa biashara hiyo haramu wanaiangamiza.
Kamanda huyo alisema kuwa siku ya Jumapili walinasa bodaboda iliyokuwa ikisafirisha misokoto 120 ya bangi katika eneo la Mteza eneobunge la Matuga.
Bw Nthege alisema bodaboda hiyo iligunduliwa katika kizuizi cha polisi.
Hata hivyo alisema aliyekuwa anasafirisha bangi hiyo alifaulu kutoroka na kuacha shehena hiyo mikononi mwa polisi.
Aidha alisema wameongeza doria za miguu kuhakikisha kuwa dawa za kulevya haziwaangamizi vijana katika eneo hilo.
Wakati huo huo aliwasuta wanaodai maafisa wa polisi wamelaza damu huku biashara ya dawa za kulevya ikikithiri.
“Maafisa wa polisi wanatekeleza wajibu wao. Jukumu la kupambana na biashara liko mikononi mwa wananchi wote. Badala ya kuwalaumu maafisa wa polisi tushirikiane kwa nyinyi kutupa habari,” akasema kamanda huyo.
Alisema kwa ushirikiano serikali ya kaunti hiyo itafaulu kuwatimua walanguzi sugu wa dawa hizo katika kaunti hiyo.
Aliwaonya wanaowaficha walanguzi akisema kuwa vijana wako katika hatari ya kuharibiwa maisha yao kutokana na utumizi wa dawa hizo.