• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Maafisa wafunga kiwanda cha kutengeneza karatasi za nailoni

Maafisa wafunga kiwanda cha kutengeneza karatasi za nailoni

Na LAWRENCE ONGARO

MAMLAKA ya Uhifadhi wa Mazingira (Nema) imefunga kiwanda kimoja eneo la Juja ambacho kimekuwa kikiendelea na biashara haramu ya utengenezaji wa karatasi za nailoni.

Hatua hiyo ilichukuliwa na ofisi ya Nema katika Kaunti ya Kiambu.

Inadaiwa kuwa kiwanda hicho kinaendesha biashara zake katika makazi ya watu, jambo ambalo ni la kuhatarisha usalama wa wakazi hao.

Naibu mkurugenzi wa Nema katika Kaunti ya Kiambu, Bw Daniel Nyamora, amesema kwamba baada ya kupokea fununu kutoka kwa wakazi wa kijiji cha Mugutha, Juja, wamechukua hatua kuvamia pahala hapo na kupata kiwanda hicho kikiendesha shughuli zake za kutengeneza karatasi za nailoni.

“Tumekuwa na changamoto tele kukabiliana na msako wa kutafuta karatasi hizo ambapo tunawapongeza wananchi kwa kutuarifu matukio yanayoendelea katika makazi yao,” alisema Bw Nyamora.

Mnamo Jumatano maafisa wa Nema walivamia kijiji hicho cha Mugutha na kupata kiwanda hicho kikiendesha biashara hiyo haramu ya kuunda karatasi za nailoni.

Alisema wakati wa uvamizi huo mmiliki wa kiwanda hicho alitoroka kwa mlango wa nyuma baada ya kupata fununu ya kwamba maafisa wa Nema wangefika hapo.

Alisema mshukiwa huyo bado anasakwa ili kuhojiwa zaidi kabla ya kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka.

Novemba 2019 Nema ilifunga kiwanda kingine eneo la Murera, Juja ambapo wafanyakazi wawili walitiwa nguvuni na kupelekwa mahakamani baadaye.

Bw Nyamora ametoa mwito kwa wakazi wa Kiambu kushirikiana na polisi na afisi yake ili kuwataja wafanyabiashara wanaoendesha biashara haramu ya kuunda karatasi za nailoni.

Kulingana na sheria iliyowekwa mfanyabiashara yeyote anayepatikana akiunda karatasi za nailoni atalazimika kutozwa Sh2 milioni ama kifungo cha mwaka mmoja hadi minne.

Bw Nyamora alisema karatasi hizo zinapata soko kubwa maeneo ya jiji la Nairobi, Thika, na Murang’a.

You can share this post!

Mwanamke aliyejeruhi wanawe kwa kisu afungwa kifungo cha...

Kapenguria Heroes wajiandalia Chapa Dimba

adminleo