• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Maafisa watatu wa ardhi ya Mavoko iliyokumbwa na ubomozi wasukumwa ndani

Maafisa watatu wa ardhi ya Mavoko iliyokumbwa na ubomozi wasukumwa ndani

Na RICHARD MUNGUTI

HATIMAYE mkono mrefu wa sheria umewakamata maafisa watatu wa kampuni ya ununuzi mashamba inayodaiwa ilinyakua shamba la ekari 4,298 ya kampuni ya kutengeneza saruji ya East African Portland Cement Company (EAPC) ya thamani ya Sh14.1 bilioni.

Watatu hao Mabw Julius Mutie Mutua, Pascal Kiseli na Alex Kyalo Mutemi walisukumwa ndani na hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Bernard Ochoi.

Bw Ochoi aliamuru Mutua, Kiseli na Mutemi wapelekwe gereza la viwandani kisha warudishwe kortini Aprili 12, 2024 mashtaka 24 ya ulaghai wa ardhi ya kampuni ya kutengeneza saruji ya EAPC.

Awali Bw Ochoi alikuwa ametoa kibali cha kuwatia nguvuni Mutua Kiseli na Mutemi kwa kutofika kortini kupokea uamuzi kuhusu ombi lao kwamba Mahakama ya Milimani haina mamlaka na uwezo wa kusikiza na kuamua kesi inayowakabili ya unyakuzi wa shamba hilo la EAPC.

Walikuwa wameomba kesi hiyo ipelekwe mahakama ya Mavoko ambapo uhalifu ulitekelezwa.

Walipokosa kufika kortini bila sababu kiongozi wa mashtaka James Gachoka aliomba mahakama itoe kibali cha kuwakamata watatu.

Mawakili wao Jackson Kala na Joseph Mutava pia hawakufika kortini.

Lakini jaribio la Bw Mutava kufutilia mbali agizo la kukamatwa kwa Mutua, Kiseli na Kyalo liligonga ukuta.

Bw Mutava alifika kortini mwendo wa saa sita unusu kuomba mahakama ifutilie mbali agizo hilo lakini akaelezwa na hakimu, “ombi la kufutiliwa mbali kwa agizo wateja wako wakamatwe laweza kusikizwa tu washtakiwa wakiwa kortini.”

Watatu hao walitarajiwa kufika kortini Machi 10, 2024 lakini ilikuwa sikukuu ya Eid Mubarak baada ya kukamilika kwa mfungo wa Ramadhan.

Bw Mutava aliwasaka watatu hao na kuwafikisha kortini saa 10 alasiri kumbe “wakati wao wa kusukumwa ndani umewadia.”

Dhamana ya Sh100,000

Bw Ochoi alifutilia mbali dhamana ya Sh100,000 waliyokuwa nje nayo kisha akaagiza wazuiliwe ndani hadi Ijumaa watakaporudishwa kusomewa mashtaka 24 ya kughushi hatimiliki ya ekari 4298 za EAPC na upokea kwa njia ya undanganyifu Sh25milioni kutoka kwa wawekezaji.

Majumba ya kifahari yaliyokuwa yamejengwa katika ardhi hiyo yalibomolewa Septemba 2023.

Ubomozi huu ulipelekea wastawishaji kuugua magonjwa ya shinikizo la damu , kisukari na wengine kadhaa kufariki kutokana na mshtuko.

Kwa muda wa miezi saba polisi wamekuwa wakichunguza kesi hiyo na wiki iliyopita Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Igonga aliamuru Mutua , Kiseli na Mutemi washtakiwe kwa ulaghai wa shamba na upokea pesa kwa njia ya undanganyifu.

Jumatatu wiki hii watatu hao waliwasilisha ombi la kuhamishwa kwa kesi hiyo kutoka Milimani hadi Mavoko, Wakili Mutava alisema kifungu cha sheria nambari 78 ya sheria za uhalifu kinasema mmoja ashtakiwe mahala uhalifu ulitendeka.

“Shamba linalodaiwa kunyakuliwa liko Athi River na kesi hii inafaa kusikizwa aidha katika mahakama ya Mavoko ama Machakos,” alisema Bw Mutava.

Watatu hao wanadaiwa walilaghai EAPC shamba hilo lenye thamani ya Sh14.1bilioni.

Mutua, Kiseli na Kyalo ambao ni maafisa  wakuu wa Aimi Ma Lukenya (AML) walifunguliwa mashtaka 24 ya kula njama kuilaghai EAPC shamba lake na kupokea kwa njia ya undanganyifu zaidi ya Sh25milioni kutoka kwa wawekezaji wakidai shamba waliyokuwa wanawauzia  ilikuwa halali.

Majumba ya kifahari yaliyokuwa yamejengwa kwenye ardhi hiyo yalibomolewa yote.

Ubomozi huo ulipelekea baadhi ya wawekazaji kufariki kutokana na mshtuko wa kupoteza rasilmali zao.

Polisi waliwakamata maafisa hao wa Aimi ma Lukenya (AML) Oktoba 2023 kufuatia kubomolewa kwa nyumba za kifahari katika eneo la Mavoko kaunti ya Machakos.

Bw Mutava alieleza mahakama kwamba shamba hilo la ekari 4,298 lenye thamani ya Sh14bilioni ilinunuliwa na wanachama wa AML.

Shamba hilo lilinunuliwa kutoka kwa kampuni inayotengeneza Saruji ya East Africa Portland (EAPC).

Lakini Mkurugenzi wa EAPC Oliver Kirubai aliyepiga ripoti alidai shamba hilo la EAPC lilivamiwa na AML.

Hakimu aliombwa na wakili Mutava awaachilie maafisa hao wa AML kwa dhamana kwa vile aki zao za kimsingi zinakandamizwa na polisi ambao wamewaonyesha cheti cha mashtaka mara mbili lakini hawajasomewa mashtaka hayo kortini.

Ijumaa Mutua, Kiseli na Mutemi watajibu “ni kweli au sio kweli waliwafuja wastawishaji zaidi ya Sh25milioni na kuilaghai EAPC shamba lake lenye thamani ya Sh14.1bn.”

  • Tags

You can share this post!

Serikali yapiga marufuku dawa ya kikohozi Benylin kufuatia...

Mahangaiko: Wakazi wanavyong’ang’ania maji...

T L