Habari Mseto

Maafisa wawafurusha wachuuzi sokoni Makongeni Thika

March 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa soko la Makongeni Thika wamefurushwa na maafisa wa polisi baada ya kudinda kufuata agizo la serikali la kujizuia kujumuika kwa vikundi.

Kwa muda wa wiki moja sasa wakazi hao ambao wengi wanaendesha biashara za vyakula katika soko hilo wamekuwa wakiendesha shughuli zao, na leo Jumanne wamefika mahali hapo bila kujali hatari inayowakaribia ya virusi vya corona.

Polisi wamevamia mahali hapo kwa vitoa machozi huku watu wakitawanyika bila kujua wanakoenda.

Wengi wao wamepata majeraha katika miili baada ya kuanguka.

Naibu kamishna wa Thika Magharibi Bw Douglas Mutai amesema hakuna njia nyingine ambayo wangetumia ila kuwafurusha na kuwajulisha umuhimu wa kuepuka kujumuika katika vikundi.

“Tumejaribu kuwasiliana nao karibu wiki moja lakini wameonekana hawakutilia jambo hilo maanani,” amesema Bw Mutai.

Amesema janga la corona ni hatari kwa usalama na hivyo halifai kufanyiwa mzaha.

“Nchi za Magharibi zina uwezo wa kimatibabu lakini sasa janga hilo linaendelea kuwalemea, je, sisi hapa tutaweza kweli na hatuna chochote cha kujivunia?” amehoji Bw Mutai.

Amesema soko hilo la Makongeni limefungwa kwa muda huku wachuuzi hao wakitafutiwa pahali pengine pa wazi wanakoweza kuendesha biashara yao.

Wakati huo pia wakazi wa kijiji cha Weteithie wameshuhudia kisa ambapo wauzaji wa mikahawa na sehemu za burudani wamefurushwa bila huruma.

Polisi wamevamia maskani hizo na kumwaga chakula kilichokuwa kimepikwa huku wakiwafurusha wenyewe kwa fujo.

Bw Mutai amesema tayari ameamuru kila mahali pafungwe kwa muda ili kujiepusha na janga la Covid-19.

Maafisa wa polisi mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Maskani 100 za kuuza pombe katika kijiji hicho zimefungwa huku wamiliki wake wakikadiria hasara watakayopata endapo hawatauza chochote.

Ametoa mwito kwa kila mmoja kufuata sheria na kunawa mikono kila mara ili kukabiliana na janga hilo.

“Kila mmoja anastahli kufuata sheria inayowekwa ya kunawa mikono kila mara bila  kuangalia mwenzako kwa sababu wewe unajilinda kibinafsi,” amesema Bw Mutai.

Bw James Wainaina ambaye ni mmiliki wa baa katika kijiji hicho cha Weteithie anasema anakadiria hasara kubwa kwa sababu kila siku yeye huwa na wateja wengi ajabu.

“Hata hivyo ni vyema kufuata sheria kwa sababu tunalinda maisha yetu kwa jumla; kwanza tupambane na janga hili halafu mengine yaje baadaye,” amesema Bw Wainaina.