• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Maajenti wa kifo: Ripoti ya NTSA bodaboda zinavyoangamiza watu  

Maajenti wa kifo: Ripoti ya NTSA bodaboda zinavyoangamiza watu  

NA PETER MBURU

WAKENYA kote nchini wako katika hatari ya kufariki, kupata majeraha au kulemazwa wakisafiri kwa pikipiki na kuacha familia zao na mzigo mkubwa wa madeni.

Watu 8,432 miongoni mwa 24,312 walioaga dunia katika ajali barabarani kati ya 2018 na 2023 walikuwa wakisafiri kwa pikipiki au walikufa baada ya kugongwa na pikipiki.

Kulingana na ripoti mpya, kwa kila Wakenya watatu waliofariki kupitia ajali za barabarani katika muda wa miaka sita iliyopita, mmoja alifariki kutokana na pikipiki ambazo zimetajaa katika barabara na mitaa nchini.

Karibu ajali 70,000 za barabarani zimefanyika nchini katika kipindi cha muongo mmoja uliopita huku Wakenya zaidi ya 120,000 wakiachwa na majeraha ya kudumu.

Kati ya 2014 na 2023, watu zaidi ya 36,000 walipoteza maisha yao kupitia ajali barabarani.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa waendeshaji pikipiki na abiria wao wako katika hatari zaidi ya kufa barabarani huku wakichangia thuluthi ya vifo vyote barabarani.

Sekta ya bodaboda imekua kwa kasi katika muda wa miongo miwili iliyopita ambapo inachangia sehemu kubwa ya uchumi wa Kenya na kuajiri maelfu ya vijana kote nchini.

Hata hivyo, wadau husika wameonya kuwa ajali za barabarani zinazohusisha waendeshaji bodaboda na wanaosafiri kwa miguu zimeongezeka kupindukia.

Mamlaka ya Usafiri na Usalama Nchini (NTSA) ilisema katika Mpango wake wa Hatua za Usalama Barabarani Nchini 2023- 2027, kuwa “baadhi ya hospitali sasa zina wadi maalum za kuhudumia wahasiriwa wa ajali za barabarani, na asilimia 80 ya wagonjwa katika hospitali walio na Majeraha ya Uti wa Mgongo ni wahasiriwa wa ajali barabarani.”

Ingawa pikipiki huchangia nafasi muhimu kwa uchumi wa nchi kwa kutoa ajira kwa vijana, kuwezesha Wakenya kufikia sehemu za mashinani ambapo magari ya kawaida hayawezi kufika, mseto wa malalamishi kuhusu wanabodaboda umevuruga sekta hiyo.

Utovu wa nidhamu ikiwemo kukiuka sheria za trafiki, mwendo kasi, kupitia sehemu zisizofaa barabarani, kunaongeza uwezekano wa ajali huku sekta hiyo ikivamiwa na wahalifu.

Jumla ya waendeshaji na abiria wa pikipiki 219 waliuawa katika muda wa wiki saba za kwanza mwaka huu (2024) idadi ambayo ni thuluthi ya vifo vya barabarani 649 vilivyoripotiwa hadi Februari 20 mwaka huu, inaeleza NTSA.

“Ni muhimu kubuni udhibiti mwafaka wa bodaboda na kuunda mikakati ya muda mrefu kuhusu usalama wa pikipiki. Hii itasaidia kuangazia tishio kadhaa zinazohusishwa na pikipiki na kuhakikisha usalama wake,” ilisema NTSA.

Wakenya 4,690 miongoni mwa 213,210 waliopoteza maisha yao 2022, waliaga dunia kutokana na ajali za barabarani kumaanisha kuwa kwa kila Wakenya 45 waliokufa mwaka huo, mmoja waliangamia kwenye ajali barabarani.

Katika muda wa wiki saba hadi Februari 20, 2024, watu 649 waliangamia barabarani katika jumla ya ajali 92 kila wiki, idadi ya juu zaidi ikilinganishwa na jumla ya vifo 83 kutokana na ajali barabarani 2023.

Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali alitoa ripoti kuhusu ukarabati wa miundomsingi ya barabarani iliyoonyesha mapengo makubwa katika usalama wa barabara wakati wa ujenzi na ukarabati, jambo ambalo huenda limechangia idadi kubwa ya ajali barabarani.

Ukaguzi huo unaashiria kuwa barabara zinazoongoza kwa idadi kubwa zaidi ya ajali mbaya barabara ni Gilgil-Mau Summit, Machakos-Kitui na Mariakani-Kaloleni-Mavueni.

Ripoti hiyo iliangazia baadhi ya visa vya ajali mbaya zaidi kushuhudiwa nchini ikiwemo ajali mbili zilizosababisha vifo vya watu 95,

Huduma ya Polisi Nchini (NPS) iliorodhesha maeneo 78 hatari zaidi kuhusu ajali za barabarani nchini.

Rekodi za NTSA zinaashiria kuwa mikasa ya barabarani inashuhudiwa kwa wingi katika barabara na kaunti fulani ambapo Nairobi, Nakuru, Machakos na Kiambu zilichangia asilimia 36 ya ajali za barabarani 2022.

  • Tags

You can share this post!

Mtandao wa wezi wanaolenga ng’ombe wa maziwa 

Kaunti zinavyoporwa kwa kukosa sajili za mali

T L