Habari Mseto

Maandamano Nakuru kulalamikia uabudu shetani shuleni

March 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

RICHARD MAOSI na MERCY KOSKEI

BAADHI ya wazazi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Jamhuri, Nakuru, Jumatatu waliandama hadi afisi ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) wakimtaka mwalimu mkuu wa shule hiyo atimuliwe kazini.

Mwalimu huyo mkuu na mwalimu mwingine wanatuhumiwa kuendeleza uabudu wa shetani, kutoza hela nyingi kupindukia na kuleta mabadiliko shuleni humo bila kuhusisha wazazi.

Wakiwa wameyabeba mabango walisababisha shughuli kusimama katikati ya mji wa Nakuru huku polisi wakiwa na wakati mgumu kudhibiti hasira za wazazi.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa wazazi wa shule hiyo Dennis Okomoll, madai wanayolalamikia ni kuibuka kwa dini ya kuabudu shetani shuleni, ubaguzi kwa msingi wa kidini, hali mbaya ya mazingira ya kusoma na miundomsingi duni.

Kulingana na wazazi, walimu wa kufunza somo la dini walitimuliwa shuleni na kupewa barua za uhamisho hadi shule zingine.

“Shule hii imekuwa na mpangilio wa kufanya maombi kila siku kabla ya ratiba ya masomo Jumatatu hadi Ijumaa,” alisema Okomoll.

Kulingana na Okomoll, mwalimu huyo mkuu amekuwa na mazoea ya kuitisha pesa kutoka kwa wazazi kabla ya kuwapa nafasi ya shule kinyume na sheria.

“Wazazi wengi wanalamikia kutozwa ada kabla ya kupewa nafasi wengine wakisema walilazimika kutoa hadi 6,000 kwa wakenya na 12,000 kwa wageni kutoka nchi jirani za Somalia na Sudan,” alisema Okomoll.

Baadhi yao waliokubali kuzungumza na ‘Taifa Leo’ wanasema walikuwa wamechoka kuwasilisha malalamishi yao kwa ofisi za (TSC) na sasa wanataka Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kuingilia kati.

Amprose Kariuki mzazi katika shule ya Jamhuri alisema hana imani na mwalimu mkuu ambaye amekuwa akipinga maombi kufanyika katika shule.

“Kusema kweli sitakubali mtoto wangu kuhudhuria shule ambayo hairuhusu maombi kufanyika ilhali tunafahamu nchi ya Kenya ina uhuru wa kuabudu,” akasema.

Kariuki anasema kama wazazi wanataka suluhisho la kudumu kwa sababu hali ya usalama wa watoto ilikuwa hatarini.

Baadhi ya walimu, wazazi na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Jamhuri, Nakuru, waandamana kulalamikia hali mbaya ya usimamizi wa shule. Wanadai kuwa mwalimu mkuu anawaingiza baadhi ya wanafunzi katika dini ya kuabudu shetani. Picha/ Richard Maosi

Kamishna wa eneo la Rift Valley George Natembeya alisema kuwa wamepokea habari hizo na kuwa wanafanya uchunguzi wao na aliwaomba wazazi wawe wakipiga ripoti kukiwa na madai ya kutozwa ada isiyofaa shuleni.

Hata hivyo, amepinga vikali watoto kuusishwa kwenye maandamano kwani kulingana na yeye wanapaswa kuwa shuleni wakisoma akisema kuwa kufanya hivo ni kukiuka haki yao ya masomo.

“Tumepokea tetesi zenyu na uchunguzi inafanywa ila tunaombwa watoto warejee shuleni kesho kwani ni hatia wao kukaa nyumbani ilhali masomo inaendelea,” alisema Natembea.

‘Taifa Leo’ haikupata fursa kuzungumza na mwalimu mkuu huyo.