Maandamano ya changarawe yazua vifo vya watu 2
STELLA CHERONO NA FAUSTINE NGILA
Usafiri kwenye barabara ya Nairobi -Narok ulikatizwa kwa muda wa saa tano Jumanne baada ya wavunaji wa changarawe kuandamana kwa madai kwamba wamiliki wa ranchi ya Kedong wameongeza ada ya kuchota changarawe kutoka Sh1,000 hadi 2,000 kwa lori moja.
Maandamano hayo yaliwaacha watu wawili wakiwa wamefariki na wengine wengi kuumia.
“Tumekuwa tukiteseka kwa kuongezwa kwa ada ya kuchota changarawe .Polisi wamekuwa wakiogoza kwenye ulafi huo,”mkazi mmoja John Simba alisema.
Wauzaji wa changarawe huwa wanalipa wenye mashamba kabla ya kuchota changarawe na kuisafirishamaeneo ya Nairobi,Nakuru,Narok na miji mingine.
Lakini Jumatatu wachota changarawe waliamkia kupata ada mpya hili likasababisha maandamano.
Maratibu wa eneo hilo la Bonde la Ufa wa usalama Gerge Natembeya alisema kwamba vijana waliweka vizuizi 20 njiani na wakaanza kudai pesa kutoka kwa magari ili wawaruhusu kupita.
“Wlikuwa wameweka vizuizi barabarani nah uku wengine wakilazimika kulipa hadi Sh 20,000 katika kila kizuizi kwani walikuwa wanadai 1,000 katika kila kizuizi,”alisema.
Kamanda wa polisi wa eneo hilo la Bonde la Ufa Marcus Ocholaa alisema kwamba alilazimika kuachilia maafisa wa GSU na ASTU ili wajrejeshe amani katika eneo hilo.