• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Mabapa mapya kuipa serikali Sh9 bilioni

Mabapa mapya kuipa serikali Sh9 bilioni

Na BERNARDINE MUTANU

Madereva watalipa serikali zaidi ya Sh9 bilioni kwa lengo la kupata mabapa ya kisasa kwa magari yao ambayo yatachukua mahali pa mabapa ya sasa katika mwaka wa kifedha unaonza Julai.

Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama(NTSA) ilisema kuwa itatoa kandarasi moja kwa moja kwa lengo la kuepuka changamoto za kisheria zilizozuia Idara ya Majela kupata kampuni inayoweza kutoa mabapa hayo.

Kila mmiliki wa gari, basi, lori au gari ndogo atalazimika kulipa Sh3,000 kupata mabapa hayo mapya, ambayo yatakuwa na kidude kilicho na uwezo wa kusoma habari kuhusiana na gari kutoka mbali.

Bw Francis Meja, Mkurugenzi Mkuu wa NTSA alisema sampuli za mabapa hayo zimesambazwa kwa makampuni ya humu nchini ili yaweze kutuma maombi ya kandarasi.

“Hatuoni sababu yoyote ya kutoa kandarasi hiyo kwa kampuni nje ya nchi kwa sababu kuna haja ya kutegemeza makampuni ya humu nchini. Tukiidhinisha kuwa yanaweza kutengeneza, tutayapa tenda hiyo,” alisema Bw Meja.

Kenya ilikuwa na magari 2.98 milioni katika barabara zake, zikiwemo pikipiki na trela mwaka wa 2017, kumaanisha serikali inatarajia Sh9 bilioni au zaidi kutokana na mabapa hayo mapya.

Hatua hiyo inalenga kumaliza wizi wa nambari za mabapa kama ilivyoshuhudiwa katika muda wa miezi kadhaa iliyokamilika, hatua inayohusisha ukwepaji wa ushuru na makundi ya kihalifu.

  • Tags

You can share this post!

Waboni 3,000 waonja utamu wa hati miliki

Leno aamini Spurs na Arsenal watatinga Nne-bora

adminleo