Habari Mseto

Mabasi 12 yaungua katika hali ya kutatanisha

August 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WAMBUI

Polisi wameanzisha uchunguzi ili kutegua kitendawili ambapo lori na mabasi 12 yanayohudumu kati ya Thika na Mombasa yaliteketea katika hali ya kutatanisha.

Magari hayo yanayomilikiwa na Sacco ya Special Travellers yaliungua Jumamosi alfajiri huku yakiwa kwenye gereji katika eneo la Kenyatta kwenye barabara kuu ya Thika.

Mmiliki wa gereji hiyo Joseph Kamau aliyepeleka maafisa wa uchunguzi katika eneo la mkasa alisema chanzo cha moto huo ni kitendawili ambacho bado hakijateguliwa.

“Nilipigiwa simu saa 8.30 usiku nikiarifiwa kuwa gereji yangu ilikuwa ikiteketea. Niliomba usaidizi kutoka kwa maafisa wa zimamoto wa Kaunti ya Kiambu. Nilipowasili katika eneo la mkasa saa 9 usiku juhudi za kuzima moto huo zilikuwa zikiendelea,” akasema.

Kwa bahati mbaya, moto huo uliteketeza mabasi 12 na lori.

“Mabasi hayo husafirisha wasafiri kutoka Thika na Nairobi hadi jijini Mombasa. Naomba polisi kuhakikisha kuwa ukweli kuhusiana na mkasa huo wa moto unabainika,” akasema Bw Kamau.

Mlinzi wa gereji hiyo alisema kuwa moto huo ulimgutusha usingizini na hafahamu chanzo chake.

“Niligutushwa usingizini na mlipuko mkubwa na nilipoamka ndipo nikagundua kuwa magari yalikuwa yakiteketea. Magari 12 yalisalia majivu,” akasema.

Mlinzi huyo alishangaa kuwa moto huo ulianzia ndani ya mabasi.

Kufikia sasa hakuna mtu amekamatwa kuhusiana na mkasa huo wa moto.