• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Mabasi 34 kusafirisha wakazi wa Baringo kuaga Moi

Mabasi 34 kusafirisha wakazi wa Baringo kuaga Moi

Na FLORAH KOECH

MABASI 34 yatatumika kusafirisha wakazi wa Kaunti ya Baringo hadi uwanja wa kitaifa wa Nyayo, Nairobi na Kabarak, Nakuru kuhudhuria hafla za mazishi ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi.

Kamishna wa Kaunti ya Nyandarua Boaz Cherutich, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya Mzee Moi Baringo alisema kuwa mabasi kumi yatatumika kusafirisha wakazi hadi Nairobi leo, ilhali 24 mengine yatatumika kusafirisha wakazi hadi Kabarak kesho, ambapo atazikwa.

Kulingana na Bw Cherutich, mipango imekamilika kuhakikisha kuwa wakazi kutoka Kaunti Ndogo sita Baringo watahudhuria hafla za kumuaga Mzee Moi, ambaye ni mzawa wa Baringo.

“Tunawataka wakazi kujitokeza mapema asubuhi ili tuhusike kumuaga kiongozi wetu,” akasema.

Uamuzi huo ulifikiwa siku chache tu baada ya wakazi wa Baringo kulalamika kwa kuwa mwili wa Mzee Moi hautapelekwa kaunti hiyo wautazame kabla ya mazishi yatakayofanyika kesho, nyumbani kwake Kabarak.

Mzee Moi alikuwa mbunge wa Baringo Kaskazini na ya Kati kwa jumla ya miaka 39 hadi alipostaafu mnamo 2002.

Alichaguliwa kuingia bunge kwa mara ya kwanza 1963 kuwakilisha Baringo Kaskazini, kisha kuanzia 1967 akawa akiwakilisha Baringo ya Kati alipohudumu hadi kustaafu. Kabla ya kujiunga na Bunge, alikuwa mwakilishi wa Bonde la Ufa katika bunge la Legco, kati ya 1955 na 1963.

Wakazi wa Baringo walilalamika kuwa licha ya kuwa alikuwa kiongozi wao kwa miaka mingi, wakazi wa eneo hilo hawakupewa fursa ya kumtazama mara ya mwisho.

“Tunaiomba serikali kuwaza kuhusu kuuleta mwili wake Kabarnet ama Sacho siku moja kabla ya mazishi kulingana na utamaduni. Huyu ni mtoto wetu na hivyo tunafaa kuhusishwa katika mipango ya mazishi yake,” akasema David Chesaro, mzee kutoka Sacho, Baringo.

Serikali ilitoa fursa kwa Wakenya kuutazama mwili wa Rais huyo Mstaafu kutoka Jumamosi hadi jana, katika majengo ya Bunge.

Mmoja wa wajukuu wa Mzee Moi, Clint Moi hata hivyo, Jumapili pia alikubaliana na wakazi wa Baringo kuwa ilifaa wapewe fursa ya kumtazama mara moja ya mwisho, alipokuwa eneo la Sacho.

“Babu yangu alikuwa Rais na hivyo mipango ya mazishi yake imetwaliwa na serikali. Hata sisi watu wa familia inatubidi kutii maamuzi ya mipango ya serikali,” akasema Clint.

You can share this post!

Hezekiah Oyugi: Katibu aliyepigiwa saluti na wakuu wa...

Jinsi nilivyomwokoa Moi alipostaafu – Francis ole...

adminleo