Mabunge ya kaunti kugoma kufuatia kutoweka kwa diwani wa Wajir Yusuf Hussein Ahmed
SHUGHULI za kawaida katika mabunge yote ya kaunti 47 zitalemazwa katika muda wa wiki mbili zijazo ikiwa diwani aliyetoweka wa Wajir, Yusuf Hussein Ahmed, hatapatikana.
Muungano wa Mabunge ya Kaunti (CAF) uliafikiana kuhusu hatua hii katika kikao chake cha majadiliano kilichofanyika jana katika hoteli ya Weston, jijini Nairobi.
Kulingana na wanachama, diwani huyo wa Wadi ya Della, hajulikani alipo kwa muda wa siku 49 zilizopita tangu alipotekwa nyara na watu wasiojulikana katika Kaunti ya Nairobi.
Mwenyekiti wa CAF, Philemon Sabulei, alisema juhudi zilizofanywa na wanachama pamoja na familia ya diwani huyo aliyetoweka hazijafanikiwa na kwamba watagoma baada ya siku 14 kushinikiza serikali kuchukua hatua.
“Tukio hili limesababisha wingu la hofu miongoni mwa madiwani kwa sababu hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kuhakikisha amerejea salama.
Licha ya kuwasiliana na Inspekta Jenerali wa Polisi na mamlaka husika mara kadhaa, hakuna hatua imechukuliwa,” alisema Bw Sabulei.
Madiwani walisema wametishiwa, kushambuliwa kimwili na kujeruhiwa na baadhi ya wabunge wanapotoa maoni yanayotofautiana katika viwango vya mashinani, ambapo wanawakilisha maslahi ya wakazi.
Madiwani wameitaka serikali, kupitia vikosi vyake vya kiusalama, kuchukua hatua ya dharura na kwa njia iliyo wazi kubainisha mahali alipo diwani aliyetekwa nyara.
Muungano huo pia uliafikiana na uamuzi kutoka kwa Spika wa Kaunti ya Wajir, Abdille Yussuf Mohamed, kuhusu kuahirisha vikao katika muda wa siku saba zijazo kama ishara ya kusimama pamoja na diwani huyo aliyetoweka, ambaye vilevile ndiye kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo.
“Kunyima Wajir haki ni kunyima haki kila sehemu ya jamhuri ya Kenya. Ni sharti tuzungumze kwa sauti ya juu na ya wazi kwamba wakati huu serikali itaheshimu uongozi wa kaunti,” alisema.
Spika Abdille alisema mwili uliopatikana ukiwa umetupwa mtoni Wajir haukuwa wa diwani aliyetoweka jinsi ilivyodaiwa na kwamba walizika mwili huo majuzi kuambatana na itikadi za kiislamu.
Alidai diwani aliyetekwa nyara yupo mikononi mwa serikali na kwamba wana sababu za kuamini serikali inahusika na tukio hilo.