• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mackenzie aomba sabuni ya kuoga na ruhusa ya kumuona mkewe gerezani

Mackenzie aomba sabuni ya kuoga na ruhusa ya kumuona mkewe gerezani

NA BRIAN OCHARO

MSHUKIWA mkuu wa mauaji ya Shakahola, Paul Mackenzie, na washukiwa wenzake 94 wameomba kupewa sabuni na bidhaa nyingine za usafi wakilalamika kuugua maradhi ya ngozi gerezani.

Kupitia kwa wakili wao, Bw Lawrence Obonyo, washukiwa hao walidai kwamba wanaugua upele kwa sababu ya uhaba wa sabuni ya kuogea.

“Inaonekana kuna mlipuko wa upele kati ya wafungwa. Wanaomba sabuni ili kudhibiti hali hiyo. Isitoshe, hawa washukiwa ni wageni wa serikali, kwa hivyo serikali inafaa kuwatunza vyema,” Bw Obonyo alisema.

Wakili huyo alimfahamisha Hakimu Mkuu wa Mombasa Alex Ithuku kwamba ugonjwa huo wa ngozi unawaathiri zaidi wanaume.

Wakati huo huo, Bw Mackenzie aliomba mahakama imruhusu kukutana na mkewe, Bi Rhoda Mumbua Maweu, ambaye pia anakabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia na anazuiliwa katika gereza la Shimo La Tewa.

Bw Obonyo alisema kuwa, wanandoa hao wanahitaji kushughulikia masuala yanayohusu watoto wao na, kwa hivyo, wanapaswa kupewa muda wa kutosha wa kukutana.

“Ni wanandoa na wana watoto. Mackenzie ameniagiza niiombe mahakama itoe amri kwa uongozi wa gereza hilo kumruhusu kukutana na mkewe. Wanataka kujadili masuala kuhusu watoto wao,” alisema wakili huyo.

Wakili huyo, hata hivyo, hakufichua zaidi juu ya aina ya mazungumzo ambayo Mackenzie anataka kuwa nayo na mkewe lakini alisema wanandoa hao hawajapata muda wa kutosha wa kuzungumza kuhusu masuala ya familia.

Zaidi ya hayo, Mackenzie ameomba kuhamishwa kutoka seli yake ya sasa hadi nyingine kutokana na msongo wa mawazo.

“Mshukiwa anaomba kuhamishwa kutoka mahali anazuiwa kwa sasa hadi nyingine kwa sababu ya msongo wa mawazo, kwa hivyo anahitaji mazingira tofauti ili kupambana na hali hiyo,” Bw Obonyo alisema.

Hakimu alikubaliana na pendekezo la wakili kwamba wanandoa hao waruhusiwe kukutana kwa ajili ya ustawi wa watoto wao na akaagiza wasimamizi wa gereza hilo wawasaidie kukutana.

Mackenzie na washukiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka 238 ya mauaji ya waumini zaidi ya 429 wa Kanisa la Good News International katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Washukiwa hao wameshtakiwa kwamba kwa kutekeleza makubaliano ya kujitoa mhanga kwa lengo la kuua, kwa pamoja waliwaua watu 238.

Wanadaiwa kutekeleza makosa hayo kwa tarehe zisizojulikana kati ya Januari 2021 na Septemba 2023 katika eneo la Shakahola huko Malindi.

Washukiwa hao wote wamekana mashtaka yote 238 ya kuua bila kukusudia.

Mackenzie na kundi lake, hata hivyo, wataendelea kuzuiliwa hadi kesi yao ya kuua bila kukusudia yatakaposikilizwa na kuamuliwa.

Hii ni baada ya Mahakama ya Mombasa kukataa jaribio lao la kupewa uhuru kwa dhamana huku wakisubiri kesi yao ianze, mapema mwezi huu.

Walinyimwa dhamana kwa vile mahakama ilibaini kuwa washukiwa hao hawana makazi ya kudumu kwa vile wote walikamatwa katika msitu wa Shakahola, hivyo itakuwa vigumu kwao kupatikana iwapo hawatafika mahakamani.

Alhamisi, upande wa mashtaka uliomba muda wa ziada wa kukusanya na kutenganisha ushahidi wake kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Mahakama imebaini kuwa inakusudia kuanza kuchukua ushahidi wa mashahidi katika kesi hiyo kuanzia Mei. Kesi hiyo itatajwa Mei 13.

  • Tags

You can share this post!

Miili ya mvulana, msichana yakwama chini ya mwamba

Majangili waua msichana na kuiba mifugo Kamologon

T L