• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Madaktari wa Cuba wavutia wagonjwa hospitalini

Madaktari wa Cuba wavutia wagonjwa hospitalini

NA KALUME KAZUNGU

IDADI ya wagonjwa wanaowasili kwenye hospitali kuu ya King Fahad, Kaunti ya Lamu imeongezeka ghafla katika kipindi cha wiki moja baada ya kuwasili kwa madaktari kutoka nchini Cuba.

Daktari Msimamizi Mkuu wa hospitali ya King Fahad, Ahmed Farid, anasema idadi ya wanaowasili kwenye hospitali hiyo kutafuta ushauri wa kimatibabu, kupimwa na kutibiwa maradhi mbalimbali kutoka kwa madaktari wa Cuba wakishirikiana na wenzao wa Lamu imeongezeka maradufu ikilinganishwa na awali ambapo madaktari hao wa kigeni walikuwa hawajawasili.

Dkt Farid anasema huenda mabadiliko hayo ya ghafla yanatokana na hamu ya wakazi kutaka kuhudumiwa na wataalamu wa kigeni.

Mapema mwezi huu, Kaunti ya Lamu ilipokea madaktari wawili wa Cuba ambao ni miongoni mwa jumla ya madaktari 100 walioletwa humu nchini na serikali ya kitaifa katika harakati za Rais Uhuru Kenyatta kuboresha sekta ya afya hapa nchini.

Dkt Farid aliwasifu wawili hao kwa bidii zao kazini.

Alitaja kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano kati ya madaktari hao wa Cuba na wagonjwa wa Lamu lakini akasema serikali ya kaunti tayari iko mbioni kuajiri mtaalamu wa kimatibabu anayefahamu lugha za madaktari hao wa kigeni ili kusaidia katika kutafsiria wagonjwa na vile vile kuwaelezea madaktari hao matatizo ambayo wagonjwa hao wangependa yatatuliwe.

Daktari Msimamizi Mkuu wa hospitali kuu ya King Fahad kaunti ya Lamu, Dkt Ahmed Farid. Asema tangu kuwasili kwa madaktari kutoka Cuba, idadi ya wanaotembelea hospitali hiyo wameongezeka maradufu. Picha/ Kalume Kazungu

Alisema ujio wa madaktari wa Cuba pia umepunguza idadi ya visa vya wagonjwa kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa kwenye hospitali za nje ya Lamu, ikiwemo Malindi, Kilifi na Mombasa.

Alisema matibabu mengi yanashughulikiwa kwenye hospitali za Lamu.

“Ujio wa madaktari wa kubwa hapa Lamu umepelekea idadi ya wagonjwa wanaotembeklea hospitali zetu kuongezeka maradufu katika kipindi cha wiki moja tangu kuripoti kwao. Wakazi wamependa sana huduma za madaktari wa Cuba. Kadhalika, madaktari wenyewe wamependa mazingira yetu.

Licha ya kuwepo kwa kizingiti cha lugha katika kuwasiliana, madaktari hao wameanza kujifunza Kiswahili ili kuwawezesha kuwasiliana na kuhudumia wagonjwa wao vyema. Isitoshe, kaunti iko kwenye harakati za kuajiri muuguzi ambaye atakuwa mkalimani kwa hawa madaktari ili kuwasiliana na wagonjwa vyema,” akasema Bw Farid.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo Jumatano walisifu huduma za madaktari hao wa kigeni na kuishukuru serikali ya kitaifa kwa kuja na mfumo kama huo wa kuajiri watalaamu kutoka nje.

“Mimi binafsi nimejihisi nimepona tayari punde madaktari wa Cuba waliponihudumia. Tunafurahia huduma zao. Tumewakaribisha Lamu na serikali iongeze idadi ya hawa madaktari Lamu. Wawili pekee hawatoshi,” akasema Bw Mohamed Famau.

  • Tags

You can share this post!

Magavana wakaangwa kutaka wasikamatwe wakiiba mali ya umma

Mbona KDF wasiondolewe Somalia? ashangaa mbunge

adminleo