• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Madaktari waonya dhidi ya kufungua shule haraka

Madaktari waonya dhidi ya kufungua shule haraka

BENSON MATHEKA na VALENTINE OBARA

MADAKTARI nchini wameonya serikali dhidi ya kuharakisha kufungua shule kabla ya kupata ushahidi dhahiri kuhusu udhibiti wa virusi vya corona.

Chama cha Matabibu nchini (KMA), kimesema kuwa, kabla ya shule kufunguliwa, ni sharti pawepo thibitisho kwamba maambukizi ya virusi vya corona katika jamii yamedhibitiwa kikamilifu.

Mwenyekiti wa chama hicho, Dkt Were Onyimo, alionya kuwa ilivyo kwa sasa, vipimo vya maambukizi ni vichache mno kwa kiwango ambacho hakiwezi kuonyesha taswira kamili ya hali ya corona nchini. Chama hicho kimetaka serikali itoe thibitisho kuwa imejiandaa kukabiliana na uwezekano wa maambukizi kuanza kuongezeka tena kwa kasi wakati shule zitakapofunguliwa.

“Chama hiki kinapendekeza kuwe na mpango ulio wazi kuhusu hatua zitkazofaa kuchukuliwa endapo kutakuwa na mkurupuko shuleni au katika taasisi nyingine za elimu,” akasema Dkt Onyimo.

Alipendekeza pia serikali itume wahudumu wa afya katika kila shule nchini kuhakikisha kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona zinazingatiwa kikamilifu, shule zitakapofunguliwa.

“Shule zilikuwa zimefungwa kwa lengo la kupunguza mtagusano na hivyo kupunguza hatari ya kueneza maambukizi ya Covid-19 nchini Kenya,” akasema.

Shule zinatarajiwa kufunguliwa kuanzia Oktoba, baada ya kufungwa kwa miezi saba kuanzia Machi. Leo, walimu wote wanatarajiwa kuwasili shuleni kwa maandalizi ya ufunguzi. Haya yanatokea wakati Rais Uhuru Kenyatta pia anatarajiwa kulegeza baadhi ya kanuni za kupambana na ueneaji wa virusi vya corona wiki hii.

Kwenye taarifa kwa wanahabari, Dkt Onyimo alisema wahudumu wa afya wanafaa kutumwa katika taasisi zote za elimu kuhudumia wanafunzi mara moja wakiugua.

Hili huenda likawa changamoto, kwani bado madaktari hulalamikia upungufu wa wahudumu wa matibabu hospitalini.

Ili kuafikia haya, chama hicho kinasisitiza kuwa ni lazima serikali iajiri wahudumu wa afya wa kutosha.

Vilevile, Dkt Onyimo alisema taasisi za elimu zinafaa kuhakikisha wanafunzi watakuwa na vifaa vya kudumisha usafi kila wakati wakiwa shuleni.

Rais Kenyatta anatarajiwa kuongoza kongamano la kitaifa kuhusu Covid-19 wiki hii, ambapo kanuni mpya za kupambana na ugonjwa huo zitatangazwa baadaye.

You can share this post!

RUTO AMNYIMA RAILA USINGIZI

‘Tangatanga’ sasa wamtaka Uhuru kuvunja Bunge