Habari Mseto

Madaktari wawili washtakiwa kuhatarisha maisha ya mgonjwa

May 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MADAKTARI wawili wa meno wameshtakiwa kuhatarisha maisha ya mgonjwa kwa kufanya kazi kiholela mwaka 2015.

Dkt Sunil Vinykak na Dkt Geoffrey Muiruri King’ang’a walikanusha mashtaka mawili yanayowakabili.

Madaktari hawa wawili ambao mahakama iliambiwa wamebobea katika taaluma ya tiba ya meno, walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bi Dolphina Alego.

Walikanusha mashtaka dhidi yao ya kumsababishia mteja wao jeraha la kudumu na kufanya kazi bila makini na kwa njia ya kiholela.

Shtaka la kwanza dhidi ya Dkt Vinyak na Dkt King’ang’a ni kwamba walimsababishia Michael Isaac Ochieng majeraha ya kudumu walipomuhudumia mnamo Agosti 26, 2015.

Upande wa mashtaka ulieleza mahakama kwamba makosa hayo yalitendeka katika hospitali yao ijulikanayo kwa jina Eurodent Centre Hospital iliyoko Westlands jijini Nairobi.

Soma Pia: Ufisadi Murang’a madaktari wakidai malipo ya huduma yatumwe kwa simu zao binafsi

Madaktari hao wa tiba ya meno wanakabiliwa na shtaka la pili la kufanya kazi bila makini na kwa njia ya kiholela.

Mahakama ilielezwa kwamba washtakiwa hao walihatarisha maisha ya Bw Ochieng waliyekuwa wamemuahidi kumtibu.

“Mnamo Agosti 26, 2015, mlihatarisha maisha ya Bw Ochieng kupitia utaratibu wa tiba mliokuwa mmeahidi kutumia. Ni kweli au sio kweli?” hakimu akawauliza washtakiwa.

“Sio kweli,” ikasikika sauti ya mmoja wa madaktari hao huku mwingine akijibu vivyo hivyo.

Mahakama iliombwa itengee kesi hiyo siku ya kusikilizwa Septemba 2024.

Wakili Pravin Bowry anayemwakilisha Dkt Vinyak alieleza mahakama atakuwa safarini kisha akaomba kesi isikizwe Septemba 3 na Septemba 4, 2024.

“Naomba hii mahakama itenge kesi hii isikilizwe kati ya Septemba 3 na Septemba 4, 2024, kuniwezesha kusafiri ng’ambo kushughulikia suala la dharura,” Bw Bowry aliomba.

Upande wa mashtaka haukupinga ombi hilo.

Bi Alego aliteua Septemba 3 na Septemba 4, 2024, siku za kusikilizwa kwa kesi hiyo dhidi ya wataalam hao wawili wa tiba ya meno.

Dkt Vinyak na Dkt King’ang’a wako nje kwa dhamana ya Sh100,000 kila mmoja.

Wawili hao walitiwa nguvuni Novemba 14, 2023, na kufikishwa kortini siku tisa baadaye mnamo Novemba 23, 2023.

Walipokamatwa, waliachiliwa na polisi kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu kila mmoja na kuamriwa wafike kortini Novemba 23, 2023.