Habari Mseto

Madawati: Magoha aonya walimu

November 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na STANLEY KIMUGE

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha ameonya maafisa wa wizara yake na walimu wakuu aliodai wanashirikiana kuiba madawati yanayonunuliwa na serikali kwa shule za umma.

Alitaja Kaunti ya Migori kama mfano wa maeneo ambapo kuna maafisa wameripotiwa kula njama ya kuiba madawati hayo, akasema wataadhibiwa.

“Ni makosa kuiba madawati kisha kuyapeleka kwingine. Kila dawati linafaa kupelekwa mahali ambapo yamepangiwa kwenda katika shule za umma,” akasema jana, alipokuwa ameenda kukagua Shule ya Msingi ya Langas, iliyo Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Serikali iliorodhesha shule 5,254 za upili na 5,136 za msingi zinazostahili kupewa madawati katika kila kaunti ndogo nchini.

Madawati yalitarajiwa kufika shuleni kabla Oktoba 19, lakini hilo halikuwezekana kwa sababu ya changamoto mbalimbali.

Prof Magoha sasa amesema serikali imo mbioni kuwasilisha madawati 653,000 kwa shule zote ifikapo Ijumaa ijayo.

“Kwa sasa tumefanikisha asilimia 60 na ninaomba maafisa wa elimu washirikiane na wenzao wa wizara ya usalama ili kuhakikisha madawati yote yanafika katika shule zinazotakikana,” akasema.

Alisisitiza kuwa uamuzi kuanzisha mpango huo ulinuiwa kunufaisha wanafunzi pamoja na maseremala wadogo. Serikali ilikuwa imetenga Sh1.9 bilioni kwa usambazaji wa madawati yanayotengenezwa humu nchini kwa shule za umma za msingi na upili. Kila shule ya msingi imepangiwa kupokea madawati 70 huku za upili zikipewa 50 kila moja.

Mpango huo unatarajiwa kushika kasi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa wanafunzi wote watahitajika kurudi shuleni ifikapo Januari 2021.