Maddison asema anastahili kuwa katika kikosi cha Uingereza baada ya kutambisha Leicester kwenye Europa League
Na MASHIRIKA
JAMES Maddison amesema anahisi kuwa tayari kurejea katika timu ya taifa ya Uingereza baada ya kufunga bao na kuchangia jingine katika ushindi wa 4-0 uliosajiliwa na waajiri wake Leicester City dhidi ya Sporting Braga ya Ureno katika Europa League mnamo Novemba 5, 2020.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 alitatizwa na majeraha mengi msimu uliopita wa 2019-20 na akakosa mechi nyingi katika kiwango cha klabu na ngazi ya timu ya taifa.
Maddison aliridhisha pakubwa katika mchuano huo uliokutanisha Leicester na Braga saa chache baada ya kutemwa na kocha Gareth Southgate katika kikosi cha Uingereza atakachokitegemea kwenye mechi mbili zijazo za UEFA Nations League dhidi ya Ubelgiji na Iceland.
“Kwa kweli inasikitisha kwamba sikuteuliwa kuunga kikosi cha Uingereza. Nilikuwa na matarajio makubwa mara hii baada ya kuachwa nje kwa mara nyingine mnamo Oktoba. Kwa sasa nimepona na niko tayari kurejea katika timu ya taifa,” akasema Maddison.
Mabao mengine ya Leicester dhidi ya Ludogorets yalifumwa wavuni kupitia kwa fowadi Dennis Praet na Kelechi Iheanacho aliyetikisa nyavu mara mbili.
Braga ambao wanajivunia tajriba kubwa katika soka ya bara Ulaya, walishuka dimbani kuvaana na Leicester wakijivunia rekodi ya kusajili ushindi mechi sita za awali.
Ushindi kwa Leicester uliendeleza rekodi nzuri ambayo imeshuhudia kikosi hicho cha kocha Brendan Rodgers kikisajili ushindi mara tano kutokana na mechi zote tano zilizopita na kupaa pia hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Leicester kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi G katika Europa League kwa alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu za mkondo wa kwanza.
Leicester kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Wolves katika mechi ya EPL itakayowakutanisha ugani King Power mnamo Novemba 8, 2020.