Madereva wamekuwa kisiki katika vita dhidi ya Covid-19 – Kagwe
Na SAMMY WAWERU
Ni vipi madereva wa malori ya masafa marefu wasio na cheti cha Covid-19 wanapita vizuizi vya maafisa wa polisi vilivyowekwa barabarani, ametaka kujua Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.
Aidha, Waziri Kagwe Alhamisi ameeleza kutilia shaka utendakazi wa maafisa wa polisi katika baadhi ya vizuizi vya barabarani nchini.
Hii ni baada ya kuibuka kuna madereva wasio na cheti cha vipimo vya Covid – 19, wanaosafirisha mizigo kutoka Mombasa hadi Busia.
Kwenye kikao na wanahabari Afya House, Nairobi, kinachoandaliwa kila siku na wizara husika kueleza hali ya virusi vya corona nchini, Bw Kagwe pia amesema kuna mchezo unaochezwa katika bandari ya mizigo Mombasa.
“Tumegundua wenye cheti cha vipimo vya Covid – 19 katika bandari ya Mombasa wanachukulia mizigo wasio na cheti. Ninashangaa madereva hao wanavyopita vizuizi vingi vya polisi barabarani bila cheti,” Waziri akasema.
“Sitaki kusema kitu. Lakini hata wewe jiulize, dereva asiye na cheti cha vipimo vya ugonjwa huu alipitaje vizuizi kutoka Mombasa hadi Busia? Ni hadithi gani wanapiga na walioko vizuizini? Iwapo umepewa jukumu la kuwa kizuizini, dereva asiye na cheti akapita, hata wewe jiulize ulikuwa umelala, ama nini ilifanyika akapita?” akaendelea kuhoji maswali yanayotilia shaka utendakazi wa maafisa wa polisi vizuizini.
Waziri alisisitiza kwamba cheti kinachokubalika ni kilichoafikia matakwa ya vipimo kwa mujibu wa maelekezo ya Shirika la Afya Duniani, ndilo WHO.
Alisema ili madereva kuruhusiwa kuondoka mipakani, lazima wawasilishe cheti cha Covid – 19 saa 48 kabla ya kuanza safari.
Wakati huohuo, Alhamisi, katika kipindi cha muda wa saa 24 zilizopita, Kenya imethibitisha maambukizi mapya 124, idadi jumla ya visa ikitimu 2,340.
Wagonjwa 39 wametangazwa kupona, idadi ya waliopona virusi vya corona nchini ikifika jumla ya 592. Hata hivyo, watu 4 wamefariki kutokana na Covid – 19, idadi jumla ya waliofariki ugonjwa huu ikigonga 78.