Habari Mseto

Madiwani wa Kericho wamkaidi Ruto, wamtimua naibu spika Erick Bett

Na VITALIS KIMUTAI November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MADIWANI wa Kaunti ya Kericho wamekaidi agizo la Rais William Ruto kwamba wakomeshe mivutano ya kisiasa katika kaunti hiyo na washirikiane na serikali ya kaunti hiyo kuwahudumia raia.

Jumatatu, siku moja baada ya kiongozi wa taifa kutoa agizo hilo na kuwaomba wasitishe mpango wa kumtimua naibu spika Erick Bett, madiwani 27 kati ya 47 walipiga kura kuunga mkono hoja ya kumtimua kiongozi huyo.

Kufuatia hatua hiyo Jumanne, katika kikao cha asubuhi cha Bunge la Kaunti ya Kericho, madiwani hao walimchagua diwani wa wadi ya Ainamoi Cheruiyot Bett kuwa naibu spika.

Uchaguzi huo uliendeshwa katika mazingira yenye utata na joto la kisiasa.

Hatua ya madiwani hao pia inaenda kinyume na maagizo yaliyotolewa na Jaji Joseph Sergon wa Mahakama Kuu ya Kericho, kuzuia Spika wa Bunge la Kericho Dkt Patrick Mutai na Madiwani kutekeleza maamuzi yaliyotokana na kutimuliwa afisini kwa Erick Bett Jumatatu.

Suala hilo sasa linausawiri uongozi wa bunge hilo, ukiongozwa Spika Mutai, kinyume na Rais Ruto aliyeagiza kuwa kikao maalum cha Jumatatu kigeuzwe cha kujadili pendekezo la kutengwa kwa ardhi katika eneo la Chelimu kwa upanuzi wa mji wa Kericho.

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kukaidi Rais ambaye pia ndiye kiongozi wa chama hicho tawala; kuhusu suala ambalo Dkt Ruto ametoa msimamo wake.

Mnamo Jumapili, Dkt Ruto alizungumzia mzozo wa uongozi katika kaunti ya Kericho akisema unadumaza maendeleo katika kaunti hiyo.

Rais alisema inachukiza kwamba baada ya kuondolewa mamlakani kwa Gavana Eric Mutai, na hatua hiyo kubatilishwa na Seneti, mvutano ungali unaendelea katika kaunti ya Kericho, madiwani wakipanga kumtimua Naibu Spika Erick Bett.

“Huu ugomvi na mivutano ni ya nini? Dakika moja, nilipokuwa nikiendelea na shughuli zangu, nilisikia Gavana ametimuliwa. Sasa nasikia mnataka kumwondoa Naibu Gavana……. Haya yote ni ya nini?Kwani hamna kazi nyingine ya kufanya?” Rais Ruto akauliza.

Alikuwa akiongea katika eneo la Kapsitet, eneo bunge la Sigowet/Soin Jumapili wakati wa ibada ya shukrani iliyoshirikisha madhehebu mbalimbali.

Rais alikariri umuhimu wa viongozi kufanyakazi pamoja na kuwahudumia wananchi ili maendeleo yaweze kufikiwa.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA