Madiwani watarajia Joho atawasikiza kikaoni
Na FARHIYA HUSSEIN
BUNGE la Kaunti ya Mombasa limepanga kuandaa kikao cha kwanza mwaka huu Jumanne huku madiwani wakitarajia Gavana Hassan Joho atahudhuria.
Kikao cha kwanza kilifaa kufanyika Februari 11, lakini kwa sababu za shughuli za kuandaa mzishi ya rais wa pili wa nchi, hayati Daniel arap Moi, kikao hicho kiliahirishwa.
Wakizungumza na Taifa Leo, baadhi ya madiwani walisema mwaka huu wanatarajia kikao cha kwanza kitahudhuriwa na gavana.
Gavana Joho anatarajiwa kusoma hotuba yake ya kila mwaka ndani ya vipindi vya kwanza mwaka huu.
Mwaka uliopita kabla ya kikao cha bunge kuenda likizo, madiwani walikuwa na majadiliano wakitaka kufahamu ni kwa nini gavana hakutoa hotuba yake ya mwaka 2019.
Hapo awali, hoja hiyo ilitolewa na diwani wa Likoni, Athman Mwamiri akimtaka Kiongozi wa wengi Bungeni, Bw Hamisi Musa kuelezea ni kwanini gavana Joho hakuonekana katika vikao vya mwaka huo wa 2019.
Bw Mwamiri alisema kuwa ni lazima Gavana kutoa hotuba yake ya mwaka kulingana na katiba ya Kaunti.
Aidha kwa upande wake Bw musa alijitetea akisema kuwa gavana alifaa kusoma hotuba yake angalau mara moja kwa mwaka.
“Gavana atatarajiwa kusoma hotuba yake baada ya kikao kurudi kutoka likizoni iliyoendwa tarehe nne mwezi wa Desemba. Bw Joho atafungua kikao cha kwanza mwaka wa 2020,” alisema Bw Musa kabla ya kikao kuenda mapumziko.
Suala jingine ambalo linafaa kujadiliwa ni ule wa mzigo kusafirishwa kupitia reli mpya (SGR).
Hapo awali madiwani walimrai gavana Joho kuzungumzia suala la SGR wakisema limewaacha wananchi wengi wa Mombasa bila kazi.
Ajenda hiyo iliwasilishwa bungeni mwezi wa Desemba mwaka 2019 kabla ya bunge kuelekea mapumziko.
Kiongozi wa wengi Bw Hamisi Musa aliwahimiza madiwani kuwa na subira akisema kuwa kuna mchakato unaoendelea na gavana atazungumzia suala hilo.
“Katibu wa kaunti anafuatilia sula hilo kwa kina, kisha gavana atapeana majibu yake,” alisema Bw Musa.
Pia, kupiga marufuku utumizi na uuzaji wa miraa ni suala ambalo linatarajiwa kugusiwa mwaka huu.
Aidha, wakazi wa Mombasa wamesubiri kwa hamu hotuba ya gavana.
“Ni muhimu gavana Joho akionyesha anatujali bado. Mengi yalishuhudiwa wakati kakao cha bunge kilienda mapumziko, kama vile uchaguzi wa mawaziri wake,” alisema Bi Mary Ann, mkazi.
Mkazi mwingine, Bw Mzee Warika alisema wamekasirishwa na jinsi kaunti inavyoendeshwa na anatumai madiwani watazungumza kwa niaba ya wakazi wote.