Habari Mseto

Mafisadi, 'hata wawili tu' watupwe jela liwe funzo kwa wengine, asema mbunge

April 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

ILI kufanikiwa, vita dhidi ya ufisadi vinafaa kuwa ni jukumu la kila mwananchi, amesema mbunge.

Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, amesema Wakenya wote wanastahili kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kupambana na ufisadi kwa sababu limekuwa donda dungu katika jamii.

“Nina hakika iwapo serikali itawasukuma gerezani mafisadi wawili pekee wenye ushawishi mkubwa serikalini, bila shaka wengine wataogopa na kuacha tabia hiyo ya uporaji wa Mali ya uma,” alisema Bw Wainaina.

Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina (mwenye maikrofoni) akiwa na wazazi wa wanafunzi wa Broadway Secondary, Thika walipopokea hundi ya karo Aprili 26, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

Alipendekeza waliopora mali ya umma wafungwe jela kwa miaka 10 ili liwe funzo kali kwa wenye tamaa ya kupora mali hiyo kiholela.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa wakati wa kukabidhi wakazi fedha za basari za wanafunzi kupitia hazina ya ustawi wa maeneobunge.

Wanafunzi wapatao 7,500 walinufaika na kitita cha Sh27.7 milioni za basari.

Baadhi ya wanafunzi walionufaika ni wale wa vyuo vikuu, shule za upili, na waliotoka katika shule za walemavu.

Alisema yeye kama mbunge aliyechaguliwa na wananchi kwa tiketi ya kujitegemea (Independent), ataendelea kumuunga Rais Kenyatta mkono kupambana na ufisadi.

“Mimi siko kwa kikundi chochote – ama mrengo wa Ruto au Kitaeleweka, na kwa hivyo nguvu zangu zote zitaelekezwa kutumikia wananchi walio nichagua,” alisema Bw Wainaina.

Aliwashutumu vikali viongozi ambao wameingiwa na tamaa ya kunyakua makaburi ya umma ya Thika.

Alisema ataungana na wakazi wa Thika kupinga unyakuzi huo.

Aliwakosoa viongozi wanaomezea mate ardhi ya ekari 635 ilyotolewa kwa Kaunti ya Kiambu na kampuni ya Delmonte.

“Ningependa kuwahakikishia wananchi ya kwamba wakazi wa Thika ni lazima wanufaike pakubwa kabla ya wengine kufaidika na ardhi hiyo,” alisema Bw Wainaina.

Aliwahimiza wananchi wafanye hima kwa kujisajili kupata Huduma Namba ili kuipa serikali nafasi ya kupanga mipango ya baadaye kwa wananchi.

“Mimi tayari nimejisajili na kwa hivyo nawahimiza wale hawajafanya hivyo kufuata mwito ili kuthibitisha uraia wao kamili,” alisema Bw Wainaina.

Alisema tayari Shule ya Msingi ya General Kago imefanyiwa ukarabati. Alipendekeza shule ya upili ya wasichana ya bweni ijengwe katika ardhi hiyo ya shule kwa lengo la kuwasajili wanafunzi wapatao 1,000.

Alipendekeza masomo ya kiufundi yatiliwe maanani katika shule ili waweze kujitegemea siku za baadaye.