Mafuriko yafukuza maafisa kutoka kituo chao cha polisi
MAAFISA wa polisi zaidi ya 30 wa Kituo cha Gamba kilicho Kaunti ya Tana River, wamehamishwa hadi katika Kituo cha Minjila baada ya kituo chao kujaa maji yanayomwagika kutoka Mto Tana.
Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo, Bw Ali Ndiema, kituo hicho kilianza kufurika Jumapili mchana.
Hata hivyo, mafuriko yaliongezeka usiku, na kufanya kituo hicho kuwa hatari kwa watu kuendelea kukitumia.
“Tulishauri maafisa wetu wahamie kituo chetu cha Kaunti Ndogo ya Minjila ambako watahudumu pamoja na wenzao hadi maji yapungue,” akasema.
Aliongeza kuwa vifaa vyote vya ofisi zimehifadhiwa na silaha zote zimehamishiwa Minjila hadi itakapokuwa salama kurudi kituoni Gamba.
Hata hivyo, alikariri kuwa maofisa wanaosimamia barabara iliyofurika watakuwa wakisafiri kwa ukaguzi wa barabara kutoka Minjila.
“Ni barabara ya kiusalama na hatuwezi kuiacha bila mtu, kwa hivyo tumejipanga ili kuhakikisha hatuna wahalifu wanaovuka,” alisema.
Pia waliohamishwa ni maafisa kutoka kambi iliyo karibu ya GSU na wakazi ambao wamekuwa wakipiga kambi kando ya barabara hiyo.
Vituo vya Polisi vya Galili na Chara pia ni miongoni mwa vituo vinavyoangaliwa, huku maji ya Mto Tana yakiendelea kumiminika hadi katika vijiji vingine.
Zaidi ya zahanati 15 pia zimeripotiwa kuzama katika kaunti nzima.
Wanafunzi wanaorejea shuleni kutoka kaunti za Lamu na Tana River pia wameathirika huku wakilazimika kutumia boti kuvuka sehemu iliyojaa maji kabla ya kupanda magari mengine kuelekea shule zao.
Kamishna wa Kaunti ya Tana River David Koskei alisema timu ya wasimamizi wa kaunti inashughulikia njia za kuhakikisha kuwa watoto kutoka shule zilizojaa mafuriko wanahudumiwa muhula unapoanza.
Katika kijiji cha Mnazini kilicho Tana River, baadhi ya wanafunzi wanalazimika kuogelea ili kufikia shule zilizo karibu katika kaunti jirani ya Kilifi.
Wanafunzi wanatumia mitumbwi kuvuka Mto Tana uliojaa mamba kwenda shuleni na kuhatarisha maisha yao.
Bw Abdallah Shehe, Polisi wa Akiba, huwa amejitolea kusaidia watoto wa shule bila malipo, kwani wazazi wengi hawawezi kulipia ada ya usafiri wa njia moja ya Sh30.
“Niliamka saa kumi na moja alfajiri ili kusaidia mke wangu na mtoto wangu kuvuka kwenda shuleni, nikaona ni vyema kuwasaidia watoto wengine hadi saa tatu asubuhi kwa kuwa sote tuko kwenye tatizo hili,” alisema.
Jioni, atakuwa hapo tena kusaidia watoto kuvuka kurudi nyumbani, jukumu ambalo ameapa kutekeleza hadi maji ya barabara ya Watta Hamesa iliyovunjika yatakapopungua na kutoa njia salama.
Afisa huyo pia anahakikisha kuwa mitumbwi inayohudumu katika sehemu hiyo haipakii watu kupita kiasi ili kuepusha ajali kama ile iliyoshuhudiwa Madogo wiki mbili zilizopita.
Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wameilaumu serikali wakisema haikuwa vyema kwa wizara ya elimu kuagiza shule zifunguliwe ilhali bado kuna sehemu za nchi zinazokumbwa na athari mbaya za mafuriko.
Watetezi hao wameapa kuchukua hatua dhidi ya Waziri wa Elimu endapo maisha yoyote ya watoto yatapotea katika ajali nyingine ya maji popote nchini.