Mafuriko yalemaza usafiri Kiserian- Magadi
STANLEY NGOTHO NA BENSON MATHEKA
MAFURIKO yamelemaza usafiri katika barabara ya Kiserian – Magadi katika siku tatu zilizopita na kuathiri wakazi na wasafiri eneo hilo.
Siku ya Ijumaa usiku, mafuriko yalizamisha barabara nyembamba ya eneo la Kamukuru na kuifanya isipitike kabisa.
Barabara hiyo ndiyo ya pekee kuingia na kutoka mjini Magadi.
Mbali na mashimo mapya, baadhi ya sehemu za barabara karibu na kambi ya Kikosi cha Kukabiliana na Fujo (GSU) zimesombwa na mafuriko.
Siku ya Jumapili, wasimamizi wa Kampuni ya Tata Chemicals walituma tingatinga kurekebisha sehemu ya barabara kuepusha madereva kukwama kwenye matope.
“Barabara nzima ilizama kutokana na mafuriko makubwa. Hatukuwa na chaguo ila kubaki nyumbani. Sehemu ya chini ya ardhi inapasuka kwa njia ya kutisha,” alisema mkazi Nancy Saruni siku ya Jumapili.
Juhudi za Mamlaka ya Barabara za Maeneo ya Mashambani Kenya (KeRRA) kurekebisha barabara katika muda wa wiki mbili zilizopita hazijafua dafu.