Habari Mseto

Mafuriko yapoteza maji jiji kuu

May 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

MITAA kadhaa katika Kaunti ya Nairobi itaendelea kukosa maji kufuatia usambazaji wa bidhaa hiyo muhimu kusitishwa ghafla na kampuni ya usambazaji maji jijini Nairobi (NCWSC).

Kwenye notisi yake, NCWSC imesema imechukua hatua hiyo baada ya mifereji ya kusambaza maji Nairobi kutoka bwawa la Sasumua kuharibiwa na maporomoko ya ardhi, kufuatia mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa.

“NCWSC imefunga kwa muda kituo cha kutibu maji cha Sasumua kinachosambaza asilimia 11.6 ya maji Nairobi. Hii ni kutokana na maporomoko ya ardhi katika Mto Karemenu ulioko katika Msitu wa Aberdare, yaliyoharibu mifereji inayosambaza maji kutoka bwawa la Sasumua,” ikaeleza.

Maeneo yaliyotajwa kuathirika kwa usambazaji wa maji ni pamoja na Lavington, maeneo karibu na barabara ya Waiyaki Way, Naivasha Road, Westlands, Parklands, Upper Hill, Kilimani, Kibra, Dagoretti Corner, Lang’ata, Kawangware na Ngando.

Mengine ni; maeneo ya Nairobi Hospital, Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta Nairobi – KNH, Chuo Kikuu cha Nairobi, Karen, Madaraka Estate, Lower Kabete, Loresho, Kitisuru, Mbagathi na Nyari, miongoni mwa mitaa mingine.

Aidha, imesema inatumia malori yake kusambaza maji mitaa iliyoathirika.

“Mafundi wetu wako eneo hilo kurekebisha hitilafu hiyo. Kwa sasa eneo hilo linashuhudia mvua kubwa, inayotatiza shughuli za usafiri kwa kuwa tutalazimika kuingia karibu kilomita 10 ndani ya msitu. Hata hivyo, serikali inafanya kila iwezalo kuangazia tatizo la ukosefu Nairobi,” notisi ya NCWSC imeeleza.

Kukatizwa kwa huduma za usambazaji maji mitaa iliyotajwa, kunajiri wakati ambapo mitaa iliyoko Thika Superhighway inaendelea kushuhudia upungufu wa bidhaa hiyo muhimu.

Wakazi wa Kasarani, Githurai, Mwiki, Zimmerman na Roysambu, wanaendelea kuhangaika ambapo wanakosa maji kwa kipindi cha zaidi ya wiki tatu sasa.

Wahudumu wa mikokoteni wanaosambaza maji, ndio wanategemewa kuyasambaza, ambapo mtungi mmoja wa lita 20 unauzwa hadi Sh50.

Uhaba unaoshuhudiwa pia umejiri wakati ambapo watu wanatakiwa kudumisha kiwango cha usafi, hasa kunawa mikono ili kuzuia maambukizi ya Covid-19.