• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Magari ya uchukuzi wa umma yatakiwa kuwa na kibali maalum

Magari ya uchukuzi wa umma yatakiwa kuwa na kibali maalum

Na SAMMY WAWERU
Imekuwa afueni kwa waliofungiwa kuingia au kutoka kaunti ya Nairobi, Mombasa na Mandera, kufuatia kutangazwa kuondolewa kwa amri hiyo mnamo Jumatatu. 
Rais Uhuru Kenyatta alisema makataa ya amri hiyo yatakamilika Jumanne Julai 7, 2020 saa kumi asubuhi.
Tangazo hilo likiwa afueni kwa waliofungiwa dhidi ya kuingia au kutoka nje ya kaunti hizo, serikali imesema magari ya uchukuzi wa umma yatakayohudumu sharti yawe yameafikia sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid – 19, unaosababishwa na virusi vya corona.
“Tukizingatia kuna uwezekano wa kusafirisha virusi kutoka eneo moja hadi lingine, hakuna matatu itakayoruhusiwa kuhudumu, kuingia na kutoka Nairobi, Mombasa na Mandera, ikiwa haijaafikia sheria na mikakati ya wizara ya afya,” Rais akasema, katika hotuba yake kwa taifa na iliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Harambee House, Nairobi kwa njia ya runinga.
Aidha, Rais Kenyatta alisema kila matatu lazima iwe na kibali cha matakwa hitajika, kusaidia kudhibiti maenezi ya virusi vya corona.
“Wahudumu lazima wawe na cheti kutoka kwa wizara ya afya kwa ushirikiano na wizara ya uchukuzi, kuonyesha wameafikia mahitaji,” akasisitiza.
Agizo hilo linawiana na la madereva wa matrela ya masafa marefu, ambao wanapasawa kuwasilisha cheti cha kupimwa Covid – 19 saa 48 kabla ya kuanza safari.
Machi 24, 2020, siku kadhaa baada ya Kenya kuthibitisha kisa cha kwanza cha corona, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa sheria na mikakati ya matatu kuzuia kuenea kwa virusi hivi, na zinazoendelea kutekelezwa.
Inajumuisha idadi ya abiria wanaosafirishwa mara moja kushushwa hadi asilimia 60 ya jumla idadi ya kiwango cha matatu, ili kuafikia kigezo cha umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mwenzake.
Isitoshe, kila matatu inapaswa kuwa na vitakasa mikono pamoja na kuhakikisha kila abiria anayeingia ana barakoa (maski).
Ni mikakati ambayo imechangia kuongezeka kwa gharama ya nauli, licha ya bei ya petroli na dizeli kupungua.
Licha ya amri ya kuingia na kutoka nje ya Nairobi na viunga vyake kuondolewa, visa vya watu kuingia na kutoka kisiri vimekuwa vikiripotiwa.

You can share this post!

Waumini wasizidi 100 makanisani – Uhuru

Matic kuchezea United hadi 2023

adminleo