Habari Mseto

Magoha awaonya Knut kwa kuvuruga mafunzo ya mtaala

April 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha ameonya Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) dhidi ya kuvuruga mafunzo ya mtaala mpya yanayoendelea nchini, huku maafisa wake wanane wakishtakiwa.

Prof Magoha alisema hatajadiliana na Katibu Mkuu wa KNUT, Wilson Sossion kuhusu mpango huo, kwani walimu hawajalazimishwa kwa vyovyote kushiriki katika zoezi hilo.

Akihutubu katika Shule ya Msingi ya Ronald Ngala, Kaunti ya Mombasa, waziri alisema masomo hayo ni muhimu, kwani yanawapa msingi bora watapoanza kuwafunza wanafunzi watakaporejea shuleni wiki ijayo.

“Huwezi kunilazimisha kufanya lolote. Hakuna mwalimu yeyote anayelazimishwa kushiriki katika mafunzo hayo. Badala yake, wanafika kwa hiari yao, kwa kuwa wanafahamu umuhimu wake. Hakuna yeyote anayepaswa kuwaambia waondoke. Atakayevunja sheria atakabiliwa vikali na polisi na kufikishwa mahakamani,” akasema Prof Magoha.

Kauli hiyo pia imetolewa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia, akisema kuwa tume hiyo itawaadhibu vikali walimu watakaovuruga mafunzo hayo.

Katika Kaunti ya Kakamega, maafisa watano wa KNUT walishtakiwa kwa kuwachochea walimu na kuvuruga zoezi la mafunzo yanayoendelea katika eneo hilo.

Watano hao wanajumuisha mwenyekiti wa KNUT katika kaunti hiyo Patrick Chungani, mwenyekiti wa Kakamega ya Kati Tom Ingolo, Kennedy Ayodi, Bi Jackline Mulindi na Bi Nelly Muliatsi.

Hata hivyo, walikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu wa Kakamega Bildad Ochieng,’ ambapo waliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 kila mmoja au Sh50,000 pesa taslimu.

Katika Kaunti ya Makueni, maafisa watatu pia walishtakiwa kwa kuvuruga zoezi hilo.

Watatu hao hata hivyo walikana mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh20,000 pesa taslimu.

Washukiwa hao walikamatwa mnamo Jumanne baada ya kuvuruga masomo hayo katika Shule ya Msingi ya Isunguluni.

Maafisa hao ni Bw Gabriel Kisilu (katibu wa tawi hilo), Bi Miriam Mwania (katibu) na Bw Henry Kivuva, anayewawakilisha walimu wa vyuo anuwai.

Katika kaunti ya Nairobi, Chama cha Walimu wa Vyuo Anuwai (KUPPET) kilisema kinaunga mkono mafunzo hayo, kwa kuwa yatawapa wanafunzi utaalamu maalum, badala ya kutilia maanani matokeo ya mitihani.

Kwenye kikao na wanahabari, mwenyekiti wa chama hicho Omboko Milemba aliusifia mfumo huo, akiutaja kama “mwanzo mpya” katika sekta ya elimu nchini.

Katika Kaunti ya Busia, katibu wa KNUT katika eneo hilo Patrick Mulamba aliachiliwa huru jana muda mfupi baada ya kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwachochea walimu wanaoendelea kupokea mafunzo kuhusu mtaala mpya.

Katibu huyo alitiwa mbaroni katika Shule ya Msingi ya Wasichana ya St. Joseph’s mjini Busia, muda mfupi baada ya kuwataka walimu wanaopokea mafunzo hayo kususia zoezi hilo.

“Huu ni msimamo wa chama kutoka kwa Bw Sossion, kuwa mafunzo hayo yasiendelee. Iwapo hawako tayari kifedha wanafaa kufahamu kuwa walimu wakuu hawatafadhili miradi ya kitaifa. Mtasalia nyumbani hadi serikali itoe marupurupu yenu,” akasema.

Na Winnie Atieno, Wanderi Kamau, Pius Maundu, Adisa Valentine Na Gaitano Pessa