• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Magoha sasa afuata nyayo za Matiang’i

Magoha sasa afuata nyayo za Matiang’i

Na PETER MBURU na FAITH NYAMAI

WAZIRI mpya wa Elimu Profesa George Magoha ameanza kazi kwa kwa kufuata nyayo za Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i za kufanya ziara za ghafla shuleni na maofisini. Bw Matiang’i alipokuwa waziri wa elimu alikuwa akitembelea wafanyakazi bila kutarajiwa.

Ijumaa, Profesa Magoha alipigwa na butwaa aliporipoti kazini na kuwakosa wafanyakazi.

Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha Profesa Magoha akiketi juu ya meza afisini akihoji baadhi ya wafanyakazi, alipobaini kuwa zaidi ya wafanyakazi 100 walikuwa wamechelewa kazini.

Mfanyakazi aliyekuwa akimtembeza kwa maana ya kuambatana pamoja na waziri huyo alikuwa na wakati mgumu kueleza kwa nini wafanyakazi hawakuwa afisini.

“Nikianza kuja hapa saa nne, hawa watu pia wataanza kuja saa nne. Si nitakasirika bure. Sharti watu wafanye kazi ama nitawafuta. Utapata wengine wanaofanya kazi. Wanaweza kwenda katika wizara ambapo wanalala,” akasema Prof Magoha.

“Hatupigani, si ni kazi tu, na mimi nafurahi nimewapata kwa kazi, lakini onyeni hao wengine,” Prof Magoha aliambia wafanyakazi waliokuwepo, ambao aliwapongeza.

Alifanya ziara hiyo Ijumaa, baada ya kuonya wafanyakazi wazembe Alhamisi kuwa wataondolewa, alipofanya mkutano siku yake ya kwanza kazini.

Ushirikiano

Prof Magoha siku hiyo aliahidi kuwa wizara yake itashirikiana na Wizara ya Usalama wa Ndani na ile ya teknolojia, kuhakikisha sekta ya elimu imenawiri nchini.

Waziri huyo aliahidi kuleta mageuzi makuu, yakiwemo kuzima kikamilifu wizi wa mitihani, kuhusisha polisi kuzima visa vya utovu wa nidhamu shuleni na kufanikisha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu.

Profesa Magoha aidha, aliahidi kuhakikisha mtaala mpya wa elimu wa 2-6-6-3-3 utatekelezwa na kufanikishwa kufikia mwaka 2020.

“Viwango vya juu vya kusimamia mitihani ya kitaifa ambavyo vilianzishwa wakati wa usimamizi wa Dkt Matiang’i katika wizara ya Elimu vitaimarishwa zaidi,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Mrengo wa Ruto wakaza kamba

Museveni amtembelea Rais Mstaafu Daniel Arap Moi

adminleo