Mahabusu alia kortini akisimulia anavyolawitiwa na wenzake seli
Na TITUS OMINDE
MAHABUSU ambaye yuko katika rumande katika gereza kuu la Eldoret alitiririkwa na machozi kortini akisimulia namna anavyolawitiwa na mahabusu na wafungwa sugu gerezani.
Mwanaume huyo alifichua mbinu chafu ambazo wafungwa hao wanatumia kumlawiti. Aliambia hakimu mkazi Stella Telewa kuharakisha kesi yake ili amnusuru kutokana na tabia ya kulawitiwa kila siku.
“Mheshimiwa wanaume ambao hawana utu gerezani wamenifanya kama mke wao ilhali mimi ni mwanaume mwenzao; wananilawiti kila siku kwa zamu. Ninaomba uharakishe kesi yangu ili nijue hatima yangu,” aliambia hakimu.
Mlalamishi huyo anakabiliwa na mashtaka ya kunajisi mtoto msichana wa umri wa miaka 16 katika mtaa wa Langas mjini Eldoret kati ya Mei 4 na 5 mwaka huu.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Septemba 19.
Hata hivyo hakimu aliagiza afisa anayesimamia gereza kuu la Elodret kufika kortini Septemba 10 kufafanua kuhusiana na madai ya kulawitiwa ambayo yalitolewa na mahabusu huyo.
“Mahakama hii inatoa agizo la kutaka afisa ambaye anasimamia gereza kuu la Elodret kufika mahakamani Septemba 10 kujibu madai ya mahabusu husika,” aliagiza hakimu.
Mahabusu mwingine ambaye jina lake tumelibana kwa usalama wake alisema kuwa tabia ya ulawiti gerezani humo ni ya kila siku wala si kitu kigeni.
Mahabusu huyo alisema visa vya kulawitiwa huripotiwa kila siku gerezani humo ambapo alisema kuna wakati mwingine wahasiriwa hupelekwa kwa matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi MTRH mjini Eldoret.
“Usiku sisi husikia watu wakilia kwa sababu ya kulawitiwa, kuna vyumba vingine ni hatari kiasi kwamba hata maafisa wa gereza huogopa kwenda katika vyumba hivyo,” alisema huku akitaka jina lake kubanwa kwa sababu za kiusalama