Mahakama Kuu yadumisha kutimuliwa kwa Malala kama Katibu mkuu wa UDA
MAHAKAMA Kuu ya Milimani, Nairobi, imedumisha kuondolewa afisini kwa seneta wa zamani wa Kakamega Cleophas Malala kama Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Mahakama hiyo pia ilikubaliana na hatua ya Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama hicho kumteua Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Bw Hassan Omar kujaza nafasi ya Bw Malala.
“Uamuzi unatolewa kuidhinisha tangazo kwenye Gazeti Rasmi la Serikali la Agosti 19, 2024 na mabadiliko katika tangazo hilo la kuondoa Bw Malala kama kaimu Katibu Mkuu na uteuzi wa Bw Omar kwa wadhifa huo sasa unasalia hivyo na ni halali,” Jaji Bahati Mwamuye akasema Jumatatu.
Alikuwa akitoa uamuzi katika kesi iliyowasilishwa na chama cha UDA kupinga uamuzi wa Jopo la Kutatua Mizozo ndani ya Vyama vya Kisiasa (PPDRT) wa kukubali rufaa iliyowasilishwa na Bw Malala na likamrejesha afisini kwa muda.
Mabadiliko hayo ya uongozi yalifanyika Agosti 2024 na ambayo yalionekana kulenga wanachama wa UDA waliosawiriwa kuwa wandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hii ni baada ya Mbunge huyo wa zamani wa Mathira kutofautiana na Rais William Ruto ambaye ni kiongozi wa kitaifa wa UDA.
Bw Gachagua, ambaye alihudumu kama naibu kiongozi wa UDA, alitimuliwa kutoka wadhifa wa naibu rais mnamo Oktoba mwaka jana na kisha akapokonywa cheo cha naibu kiongozi wa chama hicho tawala mnamo Novemba.
Naibu Rais wa sasa Kithure Kindiki ndiye alitunukiwa wadhifa huo. Bw Gachagua sasa anatarajiwa kutangaza chama chake kipya wakati wowote kuanzia Mei 1, 2025; chama kinachotarajiwa kuyeyusha umaarufu wa UDA haswa katika eneo la Mlima Kenya.
Bw Malala alipinga kuondolewa kwake akisema kuwa hakukutekelezwa kwa utaratibu uliowekwa katika chama cha UDA.
Alitaja hatua hiyo kama mapinduzi haramu na ambayo yalichochewa na kukataa kwake kumpiga vita Bw Gachagua kisiasa.
Seneta huyo wa zamani wa Kakamega aliwasilisha rufaa yake katika Kamati ya Kutatua Mizozo ndani ya UDA (IDRC) lakini juhudi zake zikagonga mwamba.