Mahakama: Shule zimeruhusiwa kuchunguza matokeo ya KCSE yaliyofutwa
Na CHARLES WASONGA
SHULE ambazo matokeo yao ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) yalifutuliwa mbali kwa madai kuwa watahiniwa walishiriki udanganyifu zitaruhusiwa kuchunguza matokeo hayo kulingana na agizo la mahakama.
Katibu katika Wizara ya Elimu anayesimamia Idara ya Elimu ya Msingi Dkt Belio Kipsang Ijumaa aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kwamba shule zote zilizotuma maombi ya kutaka kuchunguza matokeo hayo kando na kuruhusiwa kufuatilia taratibu zilizofuatwa kugundua uovu huo.
“Shule hizo zitapata nafasi ya kufuatilia mchakato huo na taratibu zote,” akasema Dkt Kipsang’ akiongeza kuwa Wizara ya Elimu itaendelea kuweka makakati madhubuti kuzuia wizi wa mitihani ya kitaifa.
Mnamo Januari mwaka huu, Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) ilifutilia mbali matokea ya wanafunzi 1,205 kutoka shule 10 kwa kushiriki udanganyifu katika mtihani huo mwaka jana.
Hata hivyo, baadhi ya shule kama Shule ya Upili ya Chebuyusi kutoka kaunti ya Kakamega, Shule ya Upili ya Wavulana ya Ortum kutoka kaunti ya Pokot Magharibi na ile ya Wasichana ya St Cecilia ziliwasilisha kesi mahakamani kupinga hatua hiyo.
Mahakama zilikubalia na maombi yao na hatua hiyo ya KNEC ikabatilishwa.
Dkt Kipsang’ aliwahakikishia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti Julius Melley kwamba wizara yake itatii agizo la mahakama kwa kuwahurusu wanafunzi na wazazi kukagua karatasi za majibu ili waelewe sababu iliyopelekea matokeo kufutuliwa mbali.