• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Mahakama yaagiza Matiang’i na Kihalangwa wamlipe Miguna Sh7 milioni

Mahakama yaagiza Matiang’i na Kihalangwa wamlipe Miguna Sh7 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MWANASHERIA mbishi Dkt Miguna Miguna aliyefurushwa kutoka humu nchini Mnamo Machi 29, 2018 atalipwa fidia ya Sh7 milioni.

Mahakama Kuu iliwaamuru Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Meja Jenerali (mstaafu) Dkt Gordon Kihalangwa wamlipe Dkt Miguna fidia hiyo wenyewe na kwa kutumia pesa za walipa ushuru.

Jaji Enoch Chacha Mwita alisema Dkt Matiang’i na Dkt Kihalangwa walikaidi maagizo ya mahakama ya kutomtimua Dkt Miguna humu nchini.

Jaji Mwita alisema Dkt Miguna ni raia wa Kenya na pasipoti aliyonayo ya nchi ya Canada “haimfanyi kuwa raia wa kigeni.”

Jaji huyo alisema maafisa hao wawili wa serikali walikaidi kifungu nambari 6 cha katiba kinachoeleza kuwa mtumishi wa umma hapasi kujihusisha katika hali itakayoletea fedheha wananchi na pia serikali.

“Fidia hii italipwa na watumishi hawa wawili wakuu wa Serikali waliokandamiza haki za mlalamishi (Miguna),” aliamuru Jaji Mwita , akiongeza, “Kamwe kodi ya umma isitumike kugharamia makosa ya wakuu hawa.”

Na punde tu baada ya mahakama kutoa agizo hilo Dkt Miguna alituma ujumbe katika mtandao wa Twitter na kusema , “Jaji Chacha Mwita amesisitiza kile nimesema kila wakati kwamba maafisa hao wawili walikandamiza haki zangu na kunivunjia heshima. Mimi ni Mkenya na sijawahi  kupokonywa uraia wangu. Ahsante Dkt John Khaminwa.”

Mawakili Cliff Ombeta (kushoto) na Nelson Havi (kulia) waliomtetea Dkt Miguna Miguna. Picha/ Richard Munguti

Aliendelea kusema ,“Haki ya mwananchi ya kuzaliwa kamwe hawezi kupokonywa. Nawapongeza Wakenya wachache walio waaminifu na pia mawakili Dkt John Khaminwa , Waikwa Wanyoike, Stephen Ongaro na wakili wa tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu -KHRC- Kamanda Mucheke pamoja na wote waliosimama nami wakati wa dhiki na tabu zangu. Nitarudi hivi karibuni. Mapambano yataendelea.”

Dkt Miguna alikamatwa na kupelekwa katika mahakama ya Kajiado kufunguliwa mashtaka kwa kumwapisha kinara wa muungano wa Nasa Raila Odinga kuwa “rais wa wananchi.”

Dkt Miguna pamoja na wakili Thomas Kajwang waliandaa taarifa ya kiapo cha Bw Odinga ambaye sasa ni ameteuliwa kusimamia Miundo Msingi barani Afrika.

Wawili hao walimwapisha Bw Odinga katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi na kuhudhuriwa na mamilioni ya wafuasi wa Nasa.

Polisi walivamia makazi ya Dkt Miguna mtaani Runda jijini Nairobi na kumpeleka mahakamani Kajiado na kutoka hapo wakampeleka usiku uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) ambapo walimlazimisha kuabiri ndege ya kwenda Dubai na kutoka hapo akasafirishwa hadi Canada anakoishi.

Polisi walikuwa wamemzuilia Dkt Miguna ndani ya seli ndogo katika uwanja wa JKIA.

“Kufurushwa kwa Dkt Miguna kulitekelezwa kinyume cha katiba na maagizo ya mahakama.Haki zake pia zilikandamizwa.” Jaji Mwita.

Akitoa uamuzi wake Jaji Mwita alisema mlalamishi alithibitisha kwamba haki zake zilikandamizwa na Dkt Matiang’i na Dkt Kihalangwa walipoamuru avurushwe hadi Canada wakidai sio raia wa Kenya.

Wakili Aaron Ndubi (kulia anayesimama) akitoa ushahidi katika kesi ya Dkt Miguna. Picha/ Richard Munguti

Mawakili James Orengo, Dkt Khaminwa, Nelson Havi , Jackson Awele , Daniel Maanzo na Otiende Amolo walimshtaki Mwanasheria Mkuu (AG), Dkt Matiang’I, Dkt Kihalangwa, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI).

Akisafirishwa kwa nguvu , Jaji Luka Kimaru alikuwa ameamuru Dkt Miguna afike kortini kujitetea dhidi ya madai alikaidi sheria kumwapisha Bw Odinga.

Wakili hiyo alimwapisha Bw Odinga kwa kushindwa uchaguzi mkuu wa 2018 akiwa na naibu wake Kalonzo Musyoka.

Jaji Mkuu David Maraga na majaji wengine sita wa Mahakama ya Juu walikuwa wamebatilisha uamuzi wa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kumtangaza Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi huo wa 2017.

Mahakama iliamuru uchaguzi wa urais urudiwe tena Oktoba 2017 lakini Bw Odinga akakataa kushiriki jambo lililopelekea ghasia kutamalaki maeneo mengi nchini Kenya.

Kaunti tano hazikushiriki katika uchaguzi huo wa urais peke yake. Mamia ya wakazi wa kaunti hizi waliuawa na polisi.

Bw Miguna kupitia vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) walipanga maandamano yaliyopelekea kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa rais wa wananchi.

Mahakama ilisema Dkt Miguna hakupasa kufurusha na kuamuru alipwe fidia ya Sh7milioni na Sh200,000 gharama ya kesi.

Agizo hili kwamba Matiang’i na Kihalangwa walipe fidia hiyo inaamaanisha hawapasi sasa kuhudumu katika nyadhifa za umma.

You can share this post!

Seneta wa zamani ajinasua seli baada ya kulipa deni

Vioja mkuu wa hospitali akijifungia ofisini asipewe barua...

adminleo