Mahakama yadinda kuwafungia wafanyakazi nje ya mtaa wa kifahari
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA Alhamisi ilitupilia mbali ombi la kuwazuia wafanyakazi wanne wa kampuni moja ya ujenzi kuingia katika mtaa wa kifahari wa Kihingo Village Waridi Gardens ulioko Kitsuru Nairobi.
Hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi alikataa ombi la wakili Jackson Ikua la kuwazuia Mabw Josiah Augo Otimo, Godfrey Ochieng Okello, Kennedy Ochieng Asewe na Shadrack Ouma Ogonji wanaoshtakiwa pamoja na mwenyekiti na mstawishaji wa mtaa aliyepia mbunge wa Tetu Bw James Ndung’u Gethenji kwa kuzua fujo mtaa huo.
Bw Ikua anayewakilisha mmoja wa walalamishi katika kesi dhidi ya wanne hao Otimo, Okello, Asewe na Ongoji alidai watawavuruga mashahidi wanaoishi katika mtaa huo wa kifahari.
Mahakama ilifahamishwa kwamba mashahidi wengi ni wakazi wa mtaa huo na “ huenda wakawatisha wasifike kutoa ushahidi katika kesi inayo wakabili ya kuhatarisha amani na kuharibu mali katika afisi za mtaa huo.
Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na mawakili Willis Otieno, Ouno Nyamweya na Ishmael Nyaribo wakisema “ kuwazuia washukiwa hao wanne ni sawa na kuwanyima riziki yao ya kila siku.”
“ Napinga vikali ombi hili. Washtakiwa hawa wanne ni wafanyakazi wa kampuni iliyopewa kandarasi ya kutekeleza kazi mbali mbali mtaani Kitsuru kujikimu kimaisha,” alisema Bw Otieno.
Wakili huyo alisema wanne hao wameajiriwa kazi na Ndung’u ambaye ni mwenyekiti na mstawishaji wa mtaa huo ambao nyumba zake ziko na thamani ya Sh20bilioni.
“ Kwa muda wa mwaka mmoja sasa tangu Oktoba 2019 washtakiwa hawa wamekuwa wakifika kortini na hakuna ripoti yoyote iliyowasilishwa na wakazi hao wa mtaa wa Kihingo katika kituo chochote cha polisi kudai wamepokea vitisho kutoka kwa washtakiwa,” alisema Bw Otieno.
Wakili huyo alisema Kifungu nambari 43 cha Katiba chatetea haki za kila mwananchi kwamba hapasi kudhulumiwa kwa njia yoyote ile.
“Kuomba wafanyakazi hawa wa Bw Gethenji wazuiliwe kuingia Kihingo kufanyakazi ili wajimudu kimaisha nikuwakandamiza haki zao wasipate chakula na fedha za kujikimu,” alisema Bw Otieno.
Akitoa uamuzi , Bw Ochoi alisema hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa kortini kuthibitisha wasahtakiwa walizua fujo au kuwatisha walalamishi.
Watano hao wanadaiwa mnamo Oktoba 16,2020 walizua vurugu.
Pia alisema wanne hao ni wafanyakazi wa Bw Gethenji aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya bunge la kitaifa na kamwe hawawezi kuzuiliwa kutekeleza majukumu yao.