• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Mahakama yampunguzia gavana dhamana kutoka Sh100m hadi Sh10m

Mahakama yampunguzia gavana dhamana kutoka Sh100m hadi Sh10m

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatano ilipunguza dhamana ya Sh100 milioni pesa taslimu aliyopewa Gavana wa Samburu, Moses Kasaine Lenolkulal hadi Sh10 milioni.

Jaji Hedwiq Ong’undi alipunguza dhamana hiyo kwa kiwango cha Sh90 milioni baada ya Bw Lenolkulal kukata rufaa akisema hangeweza kupata dhamana hiyo.

Hata hivyo Jaji Ong’udi aliamuru gavana huyo awasilishe paspoti yake mahakamani na asisafiri bila idhini ya korti inayosikiza kesi dhidi yake.

Mahakama ilisema masharti mengine aliyopewa Bw Lenolkulal na Hakimu Mkuu Douglas Ogoti yatasalia jinsi yalivyo.

Bw Ogoti aliamuru akaunti za Gavana huyo zifungwe. Ombi la kupunguza dhamana hiyo lililowasilishwa na wakili Paul Nyamondi, aliyesema dhamana hiyo ya Sh100 milioni pesa talimu inakiuka mwongozo wa dhamana uliowekwa na Idara ya mahakama.

Mwongozo huo unasema mshukiwa hafai kupewa dhamana ya kiwango cha juu kuliko pesa anazodaiwa kuiba.

Wakili huyo alikata rufaa kupinga dhamana hiyo ya kihistoria aliyopewa Bw Lenolkulal mnamo Jumanne aliposhtakiwa kwa kupokea Sh84 milioni kutoka kwa kaunti yake kinyume cha sheria.

Bw Nyamondi alisema Bw Ogoti alifikia uamuzi kwamba Gavana ni mhalifu na amefunja fedha za kaunti kwa kuruhusu kampuni yake kufanya biashara na kaunti anayoongoza.

Wakili huyo alinukuu kesi nyingine, ambapo washukiwa wanadaiwa kuiba viwango vya juu vya pesa na waliachiliwa kwa kiwango cha chini cha dhamana.

Mfano aliotoa ni kesi ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa katibu wa wizara ya spoti, Lilian Omollo aliyeshtakiwa pamoja na washukiwa wengine. Washukiwa hao waliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh1 milioni.

Pia alitoa mfano wa kesi dhidi ya aliyekuwa katibu wa wizara ya kilimo, Richard Lesiyampe aliyeshtakiwa kwa kashfa ya Sh5.6 bilioni ya mahindi na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh3 milioni.

Lenolkulal ni gavana wa pili baada ya Sospeter Ojamoong wa Busia kushtakiwa kwa ufisadi.

You can share this post!

Bunge laidhinisha Mutyambai kuwa Inspekta Jenerali mpya

Uchaguzi: ODM na Wiper tayari kumenyana Embakasi

adminleo