Mahakama yawapa wiki mbili waafikiane kuhusu kesi ya mauaji
Na RICHARD MUNGUTI
DAKTARI wa meno anataka kesi inayomkabili ya kumuua mumewe miaka 13 iliyopita iondolewe ndipo akubali kuwaondolea lawama shemejize wawili wanaoshtakiwa kwa ulaghai wa Sh700 milioni.
Wakili Justus Amareba anayemwakilisha Dkt Nisha Sapra alimweleza hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Francis Andayi kwamba, “Ninahitaji muda wa wiki mbili kuwashawishi Mabw Kuldip Sapra na Ashman Madan Sapra wamwondolee kesi ya mauaji ya Yogesh Sapra ndipo wafikie suluhu katika kesi ya umiliki wa mali wanayong’ang’ania.”
Lakini wakili Harun Ndubi anayewatetea ndugu hao alimweleza Andayi kwamba anahitaji miezi sita ndipo wafike katika mahakama kuu wakaafikiane huko jinsi ya kugawa mali ya marehemu.
“Kesi hii inasikizwa katika mahakama kuu na Jaji Aggrey Muchelule. Tunahitaji kuafikiana mbele yake ndipo tuwasilishe taarifa hapa ili kesi hii itamatishwe,” alisema Bw Ndubi.
Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alikubaliana na Bw Aremba kwamba wiki mbili zatosha kwa pande sote kuelewana.
Andayi aliwataka wote wanaohusika wafike kortini Machi 28 kueleza ikiwa wamesikizana ndipo awatengee siku ya kuamua ikiwa kesi dhidi ya Sapra na Ashman ya kughushi stakabdadhi za umiliki wa mali ya ndugu yao itaendelea au la.
“Uamuzi wangu uko tayari. Nitawasomea ikiwa hamtasikizana jinsi mtakavyoendelea,”alisema Andayi.