Habari Mseto

Mahakimu walia njaa huku majaji wakiongezewa mishahara

December 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

TUME ya kutathmini Mishahara na Marupurupu (SRC) imewaongeza mishahara majaji peke yao na kuwaacha maelfu ya mahakimu na Kadhi.

Nyongeza hii imewafanya mahakimu kulalamika na wameamua kuwasilisha kesi katika mahakama kuu kuomba walipwe mishahara mipya.

“Mahakimu na Kadhi ndio wanafanya kazi nyingi kuliko majaji na hakuna anayewajali kuwaongeza mshahara na marupupu,” alisema hakimu ambaye hakutaka jina lake litambuliwe kwa sababu za kiusalama.

“Tayari tumemwagiza wakili aishtaki SRC na JSC,” alisema hakimu huyo.

Katika taarifa iliyopelekewa msajili wa mahakama, Bi AnneAmadi mnamo Desemba 13, 2018 SRC ilikubalia tume ya uajiri watumishi wa mahakama (JSC) iwalipe majaji wa mahakama ya rufaa na mahakama kuu mishahara iliyopendekeza.

SRC ilimweleza Bi Amadi kuwa imezingatia na kuidhinisha mapendekezo ya mishahara mipya kama ilivyoiarifu katika barua ya Novemba 23, 2018.

Pia SRC imesema kufuatia msururu wa mikutano iliyofanywa Novemba 22 na Desemba 6, 2018 kuhusu suala la mishahara na marupurupu, tume hiyo imeikubalia JSC ianze kuwalipa majaji mishahara hiyo mpya.

SRC ilimweleza Bi Amadi kwamba mnamo Desemba 10, 2018 ilifanya mkutano wake mkuu na kujadilia masuala yaliyowasilishwa na JSC kuhusu nyongeza ya mishahara na kuyaidhinisha.

Tume hiyo ya mishahara ilisema kuwa imesitisha mapendekezo ya mishahara iliyokuwa imetangaza Agosti 18 mwaka uliopita kuhusu mishahara ya Majaji wa Mahakama ya Rufaa, Mahakama Kuu, Hakimu Mkuu na Hakimu Mkaazi.

Kulingana na mishahara hiyo , Jaji wa Mahakama ya Rufaa atakuwa anaanza kupokea mshahara wa Sh689,224 na kuongezwa hadi Sh1,1156,108.

Jaji wa Mahakama Kuu atakuwa anaanza na mshahara wa Sh657,426 na kuongezwa hadi Sh1,000,974.

Hakimu mkuu atakuwa anapokea Sh445,500 na kuongezwa hadi Sh727,035 na hakimu mkaazi atakuwa anapokea Sh180,000 na kuongezwa hadi kufikia Sh324,000.

Mnamo Oktoba majaji 20 waliishtaki SRC na JSC kwa kuwabagua katika malipo. Jaji George Odunga aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru isikizwe Januari 11, 2019.