Maina Njenga avamia kanisa akidai lilinyakua ardhi ya KANU
Na STEVE NJUGUNA
MGOGORO unatokota kati ya kanisa moja mjini Nyahururu, Kaunti ya Laikipia na maafisa wa chama cha Kanu eneo hilo kuhusu kipande cha ardhi.
Jumamosi iliyopita, aliyekuwa kiongozi wa kundi la Mungiki ambaye ni afisa mkuu wa Wakfu wa Amani Sasa, Bw Maina Njenga na wafuasi wake walivamia kanisa la Christian Discipleship Centre (CDC) na kulaumu viongozi wake kwa kunyakua ardhi ya afisi ya chama hicho.
Bw Njenga anayedai kuwa kiongozi wa chama cha Kanu Kaunti ya Laikipia, alisema kanisa hilo limejenga jengo la kudumu katika ardhi hiyo bila kushauriana na chama hicho.
“Rais Uhuru Kenyatta anapoendelea na vita dhidi ya ufisadi, tunapaswa kupigana na uovu huo kuanzia hapa nyumbani Nyahururu na kukomesha unyakuzi wa ardhi ili amani idumu. Ninawahimiza mpiganie ardhi hii na kuhakikisha haijanyakuliwa,” alisema Bw Njenga ambaye aligombea kiti cha useneta Kaunti ya Laikipia kwa tiketi ya Kanu na kushindwa na seneta John Kinyua.
Bw Njenga alidai kwamba kanisa lilijenga jengo hilo kwa njia isiyoeleweka na hata hailipi kodi kwa afisi ya chama.
“Hii ni mali ya chama cha KANU na wanachama wanapaswa kunufaika nayo. Tunataka kumfahamisha kiongozi wa kanisa hili hakuna njia kanisa linaweza kuhudumu katika uwanja mmoja na afisi za chama,” alisema.
Juhudi za kuzungumza na pasta wa kanisa hilo John Gacheru hazikufaulu kwa sababu hakujibu simu. Katibu wa tawi la Laikipia la chama cha Kanu David Kosgei alithibitisha kuwa chama kina mali katika miji ya Rumuruti, Karandi na Nanyuki.