Majambazi waliovaa buibui waua chifu, naibu wake
NA KALUME KAZUNGU
TAHARUKI imetanda katika kijiji cha Mbwajumwali, Kaunti ya Lamu baada ya watu wasiojulikana kuwavamia na kuwaua chifu na Naibu wake eneo hilo.
Akithibitisha mauaji hayo ya kinyama, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alisema watu waliovalia buibui na kuficha nyuso zao kwa ‘ninja’ waliingia ghafla ofisini na kuwakata kwa panga chifu Mohamed Haji Famau wa lokesheni ya Mbwajumwali na naibu wake, Malik Athman Shee wa lokesheni ndogo ya Myabogi.
Mauaji hayo yalitekelezwa majira ya saa sita adhuhuri, ambapo wauaji baadaye walitokomea kwenye msitu ulioko karibu.
Bw Macharia alisema sababu ya mauaji hayo bado haijulikani japo inakisiwa huenda waliotekeleza kitendo hicho cha kinyama ni walanguzi wa mihadarati.
Kamishna huyo alisema maafisa wa kutosha wa usalama tayari wamesambazwa kwenye eneo la Mbwajumwali na viungani mwake ili kuendeleza msako dhidi ya wahusika wa mauaji hayo.
Aliwataka wakazi kushirikiana kwa karibu na walinda usalama na kutoa ripoti zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo ya machifu.
Wakazi kwa upande wao walikuwa na wasiwasi wakihofia kuwa huenda wasio na hatia wakalengwa kwenye msako dhidi ya wahusika.