Majonzi baada ya jengo kuporomoka na kuua 4 na kujeruhi 29
Na BRIAN OKINDA na BENSON MATHEKA
WATU wanne walikufa na 29 wakapata majeraha mabaya, baada ya jengo la orofa sita mtaani Tassia, Embakasi, Nairobi kuporomoka Ijumaa asubuhi.
Jengo hilo liliporomoka mwendo wa saa mbili asubuhi huku baadhi ya wapangaji wakijiandaa kuondoka kuelekea kazini.
Afisa Mshirikishi wa eneo la Nairobi, Bw Wilson Njega, Ijumaa jioni aliambia Taifa Leo kwamba miili minne ilitolewa katika vifusi vya jengo hilo.
“Watu 29 walipelekwa katika hospitali za Mama Lucy na ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baadhi wakiwa na majeraha mabaya,” alisema.
Walionusurika walisema orofa ya chini ilizama na kisha ghorofa nyingine zikafuata mkondo. Walisema jengo hilo halijawahi kuonyesha ishara yoyote ya udhaifu na tukio hilo liliwapata wengi pasipo kutarajia.
Hata hivyo, jumba hilo ni mojawapo wa majengo mengi yaliyosongamana katika eneo la majimaji lenye idadi kubwa ya watu sawa na sehemu nyinginezo za mtaani Embakasi.
Maafisa kutoka mashirika la Msalaba Mwekundu, St John Ambulance, Idara ya Zima Moto Kaunti ya Nairobi, Polisi, na Kitengo cha Dharura cha Kikosi cha Ulinzi Kenya (RDU) walishirikiana na wakazi kuokoa watu.
Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema kupitia taarifa kuwa watu wanne waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali za Mama Lucy na Mater.
Shirika hilo lilisema familia 22 zilikuwa zinaishi katika jumba hilo.
Kihalangwa azuru eneo la mkasa
Katibu wa Kudumu katika Wizara ya Utumishi wa Umma, Bw Gordon Kihalangwa, ni miongoni mwa maafisa wa serikali waliozuru eneo hilo. Alisema jengo hilo lilikuwa na nyumba 46.
Haikubainika mara moja ni wapangaji wangapi waliokuwa ndani, janga hilo lilipotokea lakini waokoaji walihofia baadhi yao walikuwa wamekwama kwenye vifusi.
Polisi na wanajeshi wa KDF walitumia mbwa wa kunusa kuwatafuta manusura.
Mmiliki wa jumba hilo, aliyetambulishwa tu kama Mama Kanyoni, alitarajiwa kutoa rekodi za wapangaji lakini hakupatikana.
Jumba hilo liliharibu jengo jirani la mabati lililokuwa na nyumba kadhaa.
Kiini cha jengo hilo kuporomoka hakikubainika mara moja lakini mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha Nairobi na maeneo mengine nchini inatajwa kama sababu ya maafa hayo.