Habari Mseto

Majonzi watu saba wa familia wakifariki ajalini wakienda matanga

Na SIMON CIURI April 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HALI ya huzuni imetanda huko Limuru, Kaunti ya Kiambu, baada ya watu saba wa familia moja kufariki katika ajali ya barabarani karibu na mji wa Naivasha walipokuwa wakielekea kwenye mazishi ya jamaa yao.

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu jioni, Machi 31, 2025 katika eneo la High Peak kwenye barabara ya Mai Mahiu-Naivasha.

Ripoti ya polisi iliyoonwa na Taifa Dijitali inaonyesha kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gari aina ya Toyota Prado kugongana na trela.

“Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Sinotrack, lililokuwa likiendeshwa na Boniface Nyambu kutoka Mai Mahiu kuelekea Naivasha,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

“Gari lingine, lenye nambari ya usajili KBL 321K, aina ya Toyota Prado, lililokuwa likitokea upande wa pili lilijaribu kulipita gari lingine na kugongana na trela. Kutokana na ajali hiyo, abiria watatu walifariki dunia papo hapo.”

Waliopoteza maisha wametambuliwa kama Francis Muturi, dereva wa Toyota Prado, Peter Mwangi, George Ngugi, Fidelis Muturi, Cathy Wanjiru, James Kirubi, na Nimrod Munyaka, huku ripoti ikionyesha kuwa waliokufa ni pamoja na baba na wanawe watatu.

Inaripotiwa kuwa watu wawili waliokuwa ndani ya trela walinusurika bila majeraha.

“Abiria wote katika Toyota Prado walikuwa wakielekea Longonot kwa mipango ya mazishi ya jamaa mwingine,” ripoti ya polisi inaongeza.

Miili ilipelekwa katika vyumba vya kuhifadhi maiti vya Naivasha na Nakuru.

Mabaki ya gari hilo yalipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Naivasha, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.